Siku moja
Simba alikuwa akirandaranda ufukweni mwa bahari, akamwona Papa
akichomoza kichwa chake juu ya uso wa bahari katikati ya mawimbi.
Alizama na kuibuka tena… akazama na kuibuka tena… Simba alivutiwa
naye na kumwona kuwa anafaa kuwa rafiki kwani ni mkubwa na mwenye
nguvu kama yeye.
Alimwita
karibu naye akasogea.
Baada ya
kusalimiana Simba akamshauri mwenzake kuwa ipo haja ya kufanya
makubaliano ya ushirikiano na urafiki baina yao, akimchagiza kuwa
kati ya wanyama wote wa mwituni, wao Simba na Papa ndiyo wapaswao
kuwa maswahiba haswa. Kwani mmoja wao ni mfalme wa wanyama wote wa
nchi kavu ilhali mwingine ni mtawala wa viumbe wote wa baharini.
Papa
alilipokea wazo hilo la Simba kwa mikono miwili. Wakakubaliana.
Punde
akatokea Mbogo, na Simba, kwa kuwa alikuwa na njaa alimtamani na
kuanza kupambana naye. Simba alipoona analemewa aliamwita rafikiye
Papa aje nchi kavu kumsaidia.
Papa, ingawa
alikuwa na nia ya dhati ya kumsaidia, hakuweza kufanya hivyo kwani
hakuwa na namna yoyote ya kuweza kutoka majini.
Simba
akamshutumu na kumdhihaki Papa kuwa ni muasi na asiye mwaminifu.
Papa akamjibu; “Hapana rafiki yangu, wala sistahili
mzigo huo wa lawama toka kwako, yakupasa umlaumu muumba, ambaye,
pamoja na kunipa ukuu na utawala majini, ameninyima kabisa uwezo wa
kuishi juu ya nchi kavu.”
0 maoni:
Chapisha Maoni