Mtoto mmoja,
akiwa anarudi peke yake kutoka machungani wakati wa jioni, alipita
katikati ya kichaka ambako alikutana na Mbwa mwitu. Kumbe yule Mbwa
mwitu alikuwa na njaa na alijua kuwa mtoto kama yule angetosha kabisa
kwa chakula cha jioni kwake na kwa familia yake ya watoto wanne kule
pangoni. Alianza kumnyemelea akimmezea mate kwa uchu.
Yule mtoto
aliogopa sana, mwili mzima ulitetema, ingawa alijitia ujasiri na
hakutaka kufa kikondoo. Alifahamu ya kuwa hawezi kupambana naye kwa
mabavu akamshinda, wala asingeliweza kushindana naye kwa mbio
akamzidi.
Hivyo
alipoona kwamba hakuwa na namna ya kujiepusha na hatari ile,
alimgeukia Mbwa mwitu na kumwambia kwa unyenyekevu: “Najua, ee
rafiki yangu Mbwa mwitu, ya kwamba u na njaa na mimi ni windo lako,
na kwa kuwa sina uwezo wowote wa kujiokoa dhidi yako, basi kabla ya
kuniua nakuomba unisaidie kitu kimoja tu. Nacho ni uniimbie wimbo
mmoja niupendao ili nicheze kwa mara ya mwisho, kisha nikimaliza
uniue na kunila.”
Mbwa mwitu
aliangua kicheko kusikia ombi la mtoto ambaye kwake alikuwa tayari ni
marehemu mtarajiwa. Baadaye alikubali, akachukua filimbi na kuanza
kumpigia wimbo.
Wakati mtoto
anacheza huku akiwa amejawa na hofu, Mbwa wa nyumbani kwake walisikia
sauti ile, wakakimbilia pale kabla ya ule wimbo kwisha na kuanza
kumtimua yule Mbwa mwitu.
Mbwa mwitu alimgeukia mtoto akasema, “Hii ni halali
yangu; kwani mimi ambaye wasifu wangu ni muuaji na mla nyama,
sikupaswa kugeuka mpiga filimbi ili kukidhi matakwa yako wewe.”
Hadithi hii
inatufundisha nini?
1……………………………………………………………………………………………………………………
2……………………………………………………………………………………………………………………
3……………………………………………………………………………………………………………………
Taja methali, nahau au
msemo wa Kiswahili wenye maana inayofanana na maudhui ya hadithi
hii;
………………………………………………………………………………………………………………………
………………………………………………………………………………………………………………………
0 maoni:
Chapisha Maoni