Hadithi za kale zenye mafundisho za Esopo zilizoandikwa zaidi ya miaka 3000 iliyopita. Zimetafsiriwa kwa Kiswahili na Issa S. Kanguni, chini ya shirika lisilo la kiserikali la Tanzania Inventors and Techno-Thinkers Consortium (TITC). Tel; +255757242960

Tafuta katika Blogu Hii

Pages

Jumanne, 31 Desemba 2013

HADITHI YA MTOTO NA MBWA MWITU

Mtoto mmoja, akiwa anarudi peke yake kutoka machungani wakati wa jioni, alipita katikati ya kichaka ambako alikutana na Mbwa mwitu. Kumbe yule Mbwa mwitu alikuwa na njaa na alijua kuwa mtoto kama yule angetosha kabisa kwa chakula cha jioni kwake na kwa familia yake ya watoto wanne kule pangoni. Alianza kumnyemelea akimmezea mate kwa uchu.

Yule mtoto aliogopa sana, mwili mzima ulitetema, ingawa alijitia ujasiri na hakutaka kufa kikondoo. Alifahamu ya kuwa hawezi kupambana naye kwa mabavu akamshinda, wala asingeliweza kushindana naye kwa mbio akamzidi.

Hivyo alipoona kwamba hakuwa na namna ya kujiepusha na hatari ile, alimgeukia Mbwa mwitu na kumwambia kwa unyenyekevu: “Najua, ee rafiki yangu Mbwa mwitu, ya kwamba u na njaa na mimi ni windo lako, na kwa kuwa sina uwezo wowote wa kujiokoa dhidi yako, basi kabla ya kuniua nakuomba unisaidie kitu kimoja tu. Nacho ni uniimbie wimbo mmoja niupendao ili nicheze kwa mara ya mwisho, kisha nikimaliza uniue na kunila.”

Mbwa mwitu aliangua kicheko kusikia ombi la mtoto ambaye kwake alikuwa tayari ni marehemu mtarajiwa. Baadaye alikubali, akachukua filimbi na kuanza kumpigia wimbo.
Wakati mtoto anacheza huku akiwa amejawa na hofu, Mbwa wa nyumbani kwake walisikia sauti ile, wakakimbilia pale kabla ya ule wimbo kwisha na kuanza kumtimua yule Mbwa mwitu.

Mbwa mwitu alimgeukia mtoto akasema, “Hii ni halali yangu; kwani mimi ambaye wasifu wangu ni muuaji na mla nyama, sikupaswa kugeuka mpiga filimbi ili kukidhi matakwa yako wewe.”

Hadithi hii inatufundisha nini?
1……………………………………………………………………………………………………………………
2……………………………………………………………………………………………………………………
3……………………………………………………………………………………………………………………
Taja methali, nahau au msemo wa Kiswahili wenye maana inayofanana na maudhui ya hadithi hii;
………………………………………………………………………………………………………………………
………………………………………………………………………………………………………………………
Share:

Jumatatu, 30 Desemba 2013

KISA CHA SIMBA NA PANYA

Siku moja mfalme Simba akiwa amejipumzisha kivulini, alipitiwa na usingizi. Panya mtukutu alimsogelea na kuanza kuchezacheza juu yake; hali ambayo ilimfanya aamke mara moja. Alipoamka, Simba alimkamata Panya kwa kumkandamiza na guu lake kubwa, tayari kwa kumla.

Naomba unisamehe, ee Mfalme,” Panya alilia na kuomba: “nisamehe kwa sasa na sitosahau kamwe: huwezi kujua pengine ipo siku mimi pia ninaweza kulipa wema wako kwa kukusaidia!.”

Simba aliguswa sana na maneno ya Panya kwamba eti huenda ipo siku akamsaidia yeye Simba, mnyama mkubwa ambaye ni mfalme wa wanyama wote. Aliinua mguu wake na kumwacha aende zake.

Siku moja Simba alinaswa kwenye mtego wa Binadamu, na wawindaji walipomkuta walipanga kumpeleka kwa Mfalme wao kama zawadi akiwa hai vilevile. Walimfunga kwenye mti kwa kamba kisha wakaondoka kwenda kutafuta usafiri wa kumbebea.

Punde ikatokea yule Panya alipita maeneo yale, na alipomwona Simba yupo katika hali ile ya taharuki, majonzi na hofu ya kuuawa, alienda pale mtini na kuzikatakata kwa meno yake makali kamba zile zilizomfunga Mfalme wa wanyama wote.
Si nilikwambia,? unaona sasa…” alisema Panya.

Hadithi hii inatufundisha nini?
1……………………………………………………………………………………………………………………
2……………………………………………………………………………………………………………………
3……………………………………………………………………………………………………………………
Taja methali, nahau au msemo wa Kiswahili wenye maana inayofanana na maudhui ya hadithi hii;
………………………………………………………………………………………………………………………
………………………………………………………………………………………………………………………
Share:

HADITHI YA SEREMALA NA SANAMU YA MEKYURI

Kulikuwa na mtu mmoja fukara sana, kazi yake ni fundi Seremala. Ndani ya nyumba yake pamoja na vitu vingine, aliweka sanamu ya Mekyuri ambaye aliaminika kuwa ni mjumbe wa Mungu. 

Kila siku fukara huyo aliitolea sanamu ile sadaka, na kuiomba imbariki na kumfanya kuwa tajiri. Lakini fundi alizidi tu kuwa fukara siku hadi siku, zaidi na zaidi.
Mwishowe alighadhibika, akaamua kuishusha sanamu ile toka kwenye kiweko chake na kuibamiza ukutani kwa jazba.

Baada ya kichwa cha Sanamu hilo kung’oka, zikamiminika dhahabu chungu nzima, ambazo fundi Seremala alizizoa na kusema, “Ewaa, nadhani sanaa yako kwa ujumla ni ya mkanganyiko na isiyoeleweka; kwani nilipokupa heshima na kukunyenyekea sikupata mali kutoka kwako: ila sasa nimekutenda vibaya umenijazia dhahabu na utajiri tele.”

Hadithi hii inatufundisha nini?
1……………………………………………………………………………………………………………………
2……………………………………………………………………………………………………………………
3……………………………………………………………………………………………………………………
Taja methali, nahau au msemo wa Kiswahili wenye maana inayofanana na maudhui ya hadithi hii;
………………………………………………………………………………………………………………………
………………………………………………………………………………………………………………………

Share:

HADITHI YA MBWEHA NA PAKA

Mbweha alikuwa akijigamba mbele ya Paka kuwa yeye ana mbinu nyingi sana za kuwakwepa maadui zake.
Nina fuko zima la mbinu na ujanja,” alisema, “ambalo lina mamia ya njia za kujiepusha na maadui zangu wakati wa hatari.”

Mimi ninayo mbinu moja tu,” alisema Paka; “lakini ninaiamini, na inanifaa hiyo hiyo.”

Wakiongea maneno hayo, punde wakasikia sauti za Mbwa wawindaji zikielekea upande wao, na Paka alichupa akauparamia mti haraka na kujificha juu kwenye matawi. “Hii ndiyo mbinu yangu,” alisema Paka. “Je mwenzangu wafanyaje?”

Mbweha akafikiri kwanza kutumia njia hii, mara njia ile, na kabla hajafanya maamuzi, Mbwa walimkaribia na kumkaribia, na mwishowe Mbweha akiwa katika mkanganyiko huo, alikamatwa na kuuawa na Wawindaji.

Paka ambaye alikuwa akishuhudia kinachotokea, alisema;
Heri njia moja salama kuliko njia mia ambazo huwezi kuzitumia.”

Hadithi hii inatufundisha nini?
1……………………………………………………………………………………………………………………
2……………………………………………………………………………………………………………………
3……………………………………………………………………………………………………………………
Taja methali, nahau au msemo wa Kiswahili wenye maana inayofanana na maudhui ya hadithi hii;
………………………………………………………………………………………………………………………
………………………………………………………………………………………………………………………
Share:

KISA CHA SUNGURA NA SIMBA

Hapo zamani za kale kulikuwako mkutano mkuu wa wanyama kila baada ya miaka mitatu, ambapo wanyama wote walipata fursa ya kutoa michango ya mawazo ili kuboresha kanuni na namna ya maisha yao kama jamii moja.

Siku moja, wakiwa katika mkutano kama huo, Sungura walitoa mawaidha kwa hisia kali sana, rai yao ikiwa ni kutaka wanyama wote wawe na haki sawa.

Tunataka haki sawa kwa wanyama wote, wakubwa kwa wadogo, wala nyama kwa wala nyasi…”

Simba ambaye alikuwa ndiye mwenyekiti wa mkutano akawajibu: “maneno yenu, enyi Sungura! ni mazuri sana; ila hayana makucha wala meno kama tuliyonayo sisi.”

Hadithi hii inatufundisha nini?
1……………………………………………………………………………………………………………………
2……………………………………………………………………………………………………………………
3……………………………………………………………………………………………………………………
Taja methali, nahau au msemo wa Kiswahili wenye maana inayofanana na maudhui ya hadithi hii;
………………………………………………………………………………………………………………………
………………………………………………………………………………………………………………………
Share:

HADITHI YA SIMBA NA SUNGURA

Simba mwenye njaa, katika pitapita zake za kuwinda, alimkuta Sungura akiwa amelala fofofo. Alishusha pumzi, akatabasamu na kumshukuru sana Mungu kwa ukarimu wake wa kutambua taabiko lake na kumtunuku chakula pasi na haja ya kukitolea jasho.

Taratibu alimsogelea Sungura ili asije akamwamsha, akalala yeye…
Alipoinua miguu yake kutaka kumkamata, mara akatokea Ayala mnono ambaye alipita akikimbia karibu naye, akielekea upande wa kaskazini kwenye uwanda wa nyasi fupi.

 Simba alimwacha Sungura na akakurupuka kumkimbiza yule Ayala.
Vishindo kelele na purukushani za Simba na Ayala vilimgutusha na kumwamsha Sungura ambaye aliamka na kutimua mbio kuelekea upande wa kusini.

Baada ya kumkimbiza Ayala kwa muda mrefu Simba alishindwa na kuamua kurudi ili akamle yule Sungura.
Alipogundua kuwa Sungura naye alikuwa ameamka na kukimbia, Simba alisema kwa kujilaumu, “ama kweli nimepata nilichostahili; kwa kuwa nilikiacha chakula nilichokitia mkononi tayari kwa tamaa ya kutaka kupata zaidi.”

Hadithi hii inatufundisha nini?
1……………………………………………………………………………………………………………………
2……………………………………………………………………………………………………………………
3……………………………………………………………………………………………………………………
Taja methali, nahau au msemo wa Kiswahili wenye maana inayofanana na maudhui ya hadithi hii;
………………………………………………………………………………………………………………………
………………………………………………………………………………………………………………………
Share:

HADITHI YA MTU NA MTI

Mtu mmoja alikwenda kichakani huku akiwa na shoka mikononi kwake, na kuiomba Miti kwa unyenyekevu ili iweze kumpa tawi moja tu dogo ambalo alisema alikuwa na kazi nalo fulani.

Miti ile ilikuwa na tabia njema, ikampa moja ya matawi yake. Kumbe yule mtu alikuwa akihitaji mpini wa shoka lake. Kwa kutumia tawi lile alilopewa akakarabati shoka lake na kisha kuanza kazi ya kuikata Miti ile mmoja baada ya mwingine.

Ndipo Miti ilipon’gamua ilitenda ujinga kwa kiasi gani kutokana na kitendo kile cha kumsaidia adui yao mpini, ambao ulitumika kulitengeneza shoka, ambalo lilitumika kuiangamiza Miti yenyewe.

Hadithi hii inatufundisha nini?
1……………………………………………………………………………………………………………………
2……………………………………………………………………………………………………………………
3……………………………………………………………………………………………………………………
Taja methali, nahau au msemo wa Kiswahili wenye maana inayofanana na maudhui ya hadithi hii;
………………………………………………………………………………………………………………………
………………………………………………………………………………………………………………………
Share:

HADITHI YA NYANI NA WANAWE MAPACHA

Ilisemekana wakati fulani kuwa Nyani mmoja alikuwa akizaa watoto wawili mapacha katika kila mzao wake. Na alikuwa na kasumba ya kumpenda na kumjali sana mtoto mmoja, yule mdogo, huku akimchukia na kutomjali kabisa yule mkubwa.

Ikatokea katika mzao wake mmoja kwamba yule mdogo aliyempenda na kumjali akasongwasongwa na kudhoofika kiafya na kimaadili kutokana na upendo wa mamaye uliopita kiasi, wakati yule mkubwa aliyechukiwa alipata mafundisho na kustawi licha ya kuishi maisha ya kutojaliwa na kuchukiwa na mama yake.

Hadithi hii inatufundisha nini?
1……………………………………………………………………………………………………………………
2……………………………………………………………………………………………………………………
3……………………………………………………………………………………………………………………
Taja methali, nahau au msemo wa Kiswahili wenye maana inayofanana na maudhui ya hadithi hii;
………………………………………………………………………………………………………………………
………………………………………………………………………………………………………………………
Share:

KISA CHA SIMBA, MBWA MWITU NA MBWEHA

Simba, kutokana na uzee wake, alilala akiwa hoi mgonjwa kwenye pango lake. 
Wanyama wote wa mwituni walikwenda kumwona na kumsalimu mfalme wao, isipokuwa Mbweha. Kwahiyo Mbwa mwitu, ambaye walikuwa na uhasama wa jadi na Mbweha, aliwaza kuwa huo ulikuwa ni wasaa mzuri sana wa kumkomoa. Akabuni hila ya kutoa mashtaka kwa Mfalme Simba kwamba Mbweha hakuwa na adabu kwake yeye ambaye ni mfalme wao wote na kwamba hakuwa na sababu yoyote ya kutokuja kumjulia hali.

Wakati huohuo Mbweha naye akaingia mle ndani na kuyasikia maneno ya Mbwa mwitu kwa Simba. Simba alimwona na akanguruma kwa ghadhabu dhidi yake. Ndipo Mbweha naye akaona huo ulikuwa ni wasaa wake wa kujitetea na kumgeuzia kibao adui yake, akasema,
ee bwana Mfalme mkuu, hivi ni nani kati ya wote waliokuja kukuona katika hali yako ya ugonjwa wamekuwa wa msaada mkubwa kwako kama mimi, ambaye nimesafiri nchi na nchi, nikaelekea kila upande, nikitafuta na kujifunza toka kwa matabibu dawa ya kukuponya ewe Mfalme wangu?”

Simba akamwamuru amtajie dawa hiyo aliyoigundua mara moja; kabla hajafikiria adhabu ya kumpa kutokana na kuchelewa kwake kuja kumjulia hali Mfalme.

Mbweha akajibu; “Dawa ya kukuponya ee Mfalme ninaijua, na ni ya uhakika kabisa. Itakulazimu ufanye ifuatavyo; Umchune Mbwa mwitu angali yu hai na kisha ujitande ngozi yake ingali ya vuguvugu. Utapona kabisa maradhi yako, na pia utaishi miaka mingi bila kupatwa kamwe na ugonjwa kama huu.”

Simba, kutokana na mateso aliyoyapata na hali mbaya aliyokuwa nayo wakati ule, alijikuta akipata tumaini ghafla kwa dawa ile ya Mbweha. Japo hakuwa na uhakika nayo, alitaka kuijaribu ili aokoe maisha yake.

Mbwa mwitu alikamatwa mara moja na akachunwa ngozi kikatili akiwa hai; ilhali Mbweha alimgeukia, akamwambia huku akitabasamu, “Ulipaswa kumfariji Mfalme wako kwa maneno mazuri ya faraja na kumtia moyo badala ya maneno ya fitina yenye kuchukiza na kukera.”

Hadithi hii inatufundisha nini?
1……………………………………………………………………………………………………………………
2……………………………………………………………………………………………………………………
3……………………………………………………………………………………………………………………
Taja methali, nahau au msemo wa Kiswahili wenye maana inayofanana na maudhui ya hadithi hii;
………………………………………………………………………………………………………………………
………………………………………………………………………………………………………………………

Share:

KISA CHA MWANAFALSAFA, MCHWA NA MEKYURI

Hapo zamani za kale, Mwanafalsafa mmoja alikuwa na kawaida ya kwenda ufukweni mwa bahari kila siku nyakati za jioni, kujipumzisha na kutafakari. Ikatokea alasiri ya jumamosi moja, akiwa ufukweni kama ilivyo ada yake, alishuhudia kwa macho yake mashua ikipigwa na dhoruba kali na kuzama.
Mabaharia na abiria wote waliokuwamo chomboni walizama na kufa maji. 

Yule bwana alihuzunika sana, hata alifikia kulaani kwamba majaaliwa ya Mungu hayakuwa ya haki kwani kutokana na mtu mmoja tu ambaye alipaswa kufikwa na mauti siku ile, umati mkubwa uliangamizwa pamoja naye. “Iweje roho za watu wote wale ziangamizwe kwa ajili ya mtu mmoja tu ambaye alipaswa kufa leo?” alijiuliza akiinua mikono yake juu kama ishara ya lawama kwa Mungu.

Wakati akiendelea kutafakari mawazo yake hayo, mara akajikuta amezungukwa na jeshi zima la Mchwa, ambao kumbe alikuwa amesimama kando ya nyumba yao.
Mmojawapo kati ya mchwa waliompanda miguuni alimng’ata na kumsababishia maumivu makali sana.
Yule bwana alighadhibika na kuanza kuwapondaponda kwa miguu na kuwaua mchwa wote waliokuwapo karibu naye.

Mara Mekyuri alitokea, akamcharaza fimbo za maonyo yule Mwanafalsafa huku akisema, “uu nani wewe hata ukatoa hukumu juu ya matendo ya Mungu juu ya wanadamu, ilhali wewe mwenyewe unatenda vivyo hivyo kwa Mchwa?”

Hadithi hii inatufundisha nini?
1……………………………………………………………………………………………………………………
2……………………………………………………………………………………………………………………
3……………………………………………………………………………………………………………………
Taja methali, nahau au msemo wa Kiswahili wenye maana inayofanana na maudhui ya hadithi hii;
………………………………………………………………………………………………………………………
………………………………………………………………………………………………………………………
Share:

Jumatatu, 23 Desemba 2013

KISA CHA MBWEHA, JOGOO NA MBWA

Kulitokea usiku mmoja wa mbalamwezi Mbweha alikuwa akizungukazunguka kwa mawindo kwenye shamba la Mkulima mwenye mifugo, ambapo aliliona Jimbi moja limesimama juu kabisa asipoweza kufikia likiwika kwa sauti ya juu.
Habari njema, habari njema!” Mbweha alipaza sauti kwa hila.
Nijuze, ni ipi habari hiyo njema?” Jimbi lilijibu.

Mfalme Simba ametoa tamko la makubaliano ya amani kwa wanyama wa ulimwengu mzima. Kuanzia sasa ni marufuku kwa mnyama yeyote kumdhuru mwingine, bali sote hatuna budi kuishi pamoja kwa amani na urafiki kama ndugu.”
Shime, hakika hiyo ni habari njema,” lilisema Jimbi; kisha likaendelea “na kule kwa mbali namwona kuna rafiki anakuja, ambaye tunaweza kufurahi naye pamoja, tukianza ukurasa huu mpya wa amani.” Akisema hayo Jimbi aliinyoosha shingo yake akitazama mbali upande ule alio yule mbweha.

Unamwona nani anakuja?” Mbweha aliuliza kwa hamaki.
Ni Mbwa wa bwana wangu ndiye anayekuja kuelekea upande wetu… Vipi, mbona unaondoka mapema?” aliuliza, kwani Mbweha alishageuka na kuanza kuondoka mara baada ya kusikia habari ya ujio wa Mbwa.

Huwezi kusubiri kidogo umpongeze Mbwa kwa kupata utawala wa sheria hii mpya ya amani ya ulimwengu?” alimuuliza huku akitabasamu.
Ningeliweza kufanya hivyo,” alijibu Mbweha, “ila nahofia huenda Mbwa akawa hajasikia bado tangazo la mfalme Simba.”

Hadithi hii inatufundisha nini?
1……………………………………………………………………………………………………………………
2……………………………………………………………………………………………………………………
3……………………………………………………………………………………………………………………
Taja methali, nahau au msemo wa Kiswahili wenye maana inayofanana na maudhui ya hadithi hii;
………………………………………………………………………………………………………………………
………………………………………………………………………………………………………………………
Share:

KISA CHA MWANAMFALME NA PICHA YA SIMBA

Hapo zamani kulikuwako Mfalme, ambaye alikuwa na mtoto mmoja tu wa kiume, kijana aliyependa sana mazoezi ya sanaa za mapigano. Kila siku alijichanganya na vijana wa rika lake katika mazoezi na michezo. Na awapo nyumbani alipendwa sana na wazazi wake, hasa baba yake.

Siku moja Mfalme akiwa usingizini aliota ndoto. Na katika ndoto hiyo alipewa onyo la kuwa mwanaye huyo wa pekee atakufa kwa kuuawa na kuliwa na Simba.
Aliposhtuka alipatwa na hofu, kwani katika himaya yake wanyama wakali kama Simba kushambulia binadamu au mifugo ilikuwa kawaida.
Kwa kuhofia huenda ndoto yake ikawa ni ujumbe wa kweli, aliamua kumjengea yule mwanaye, Mwanamfalme, kasri kubwa maridadi.

Jengo lilinakshiwa maridadi na kuta zote zilipambwa kwa picha nzuri za wanyama mbalimbali, zikiwa na ukubwa unaolingana na wa wanyama halisi. Mojawapo kati ya zile picha za ukutani ilikuwa ni picha ya Simba dume.
Hivyo Mwanamfalme aliwekwa ndani ya kasri, akapewa mahitaji yote humo, akafungiwa asitoke nje hata mara moja kwa hofu ya kuuawa na Simba.

Siku moja yule kijana mwana wa mfalme aliiona ile picha ya Simba, ndipo huzuni yake ya kukosa uhuru na kufungiwa ikafufuka upya, na akiwa amesimama kando ya ile picha ya Simba, aliitazama kwa jazba na kusema: “ee mnyama ninayekuchukia kuliko wanyama wote! Kutokana na ndoto ya uwongo aliyoota baba yangu, na kuona maono ya usingizini, nimefungiwa ndani ya kasri hili kama mtoto wa kike, nisitoke kwa kukuhofia wewe: nikutende nini sasa baradhuli mkubwa wee?” Akisema hivyo aliunyoosha mkono wake wa kuume kuelekea mti wa miiba, kwa nia ya kukata tawi atengeneze fimbo ili amsulubu yule Simba kwa kisasi.

Bahati mbaya miba moja ilimchoma kidoleni, akatokwa damu nyingi na kupata maumivu makali sana, kiasi kwamba Mwanamfalme alianguka chini na kuzirai. Ghafla alishikwa na homa kali, ambayo ilimuua siku chache baadaye.

Hadithi hii inatufundisha nini?
1……………………………………………………………………………………………………………………
2……………………………………………………………………………………………………………………
3……………………………………………………………………………………………………………………
Taja methali, nahau au msemo wa Kiswahili wenye maana inayofanana na maudhui ya hadithi hii;
………………………………………………………………………………………………………………………
………………………………………………………………………………………………………………………
Share:

KISA CHA KIJANA NA UPUPU

Hapo zamani kulikuwa na Kijana mmoja mtukutu ambaye alipenda sana kuchezea mimea na wadudu. Siku moja akiwa kwenye kichaka jirani na nyumbani kwake, aligusa Upupu kwa mkono wake wa kuume, nao ukaanza kumwasha. Ukamletea karaha na maumivu makali.

Akaamua kukimbilia nyumbani kwake haraka huku akiendelea kujikuna na machozi yakimlengalenga. Alimfuata Mama yake bustanini na kumwambia kwa sauti ya kudeka akisema,
Mama, Ingawa upupu unanichomachoma na kuniletea maumivu makali kiasi hiki, mie niliugusa taratibu na kwa unyenyekevu. Sijui ni kwa nini unaniumiza hivi”
Kuugusa taratibu ndiyo haswa sababu iliyopelekea ukuchome, na kukuumiza.” Mama yake alimwambia. “Siku nyingine mwanangu, ukitaka kuugusa Upupu, ukamate na uufinye kwa nguvu, nao utakuwa laini na mororo kiganjani mwako, na wala hautokuchoma na kukuumiza hata kidogo.”

Hadithi hii inatufundisha nini?
1……………………………………………………………………………………………………………………
2……………………………………………………………………………………………………………………
3……………………………………………………………………………………………………………………
Taja methali, nahau au msemo wa Kiswahili wenye maana inayofanana na maudhui ya hadithi hii;
………………………………………………………………………………………………………………………
………………………………………………………………………………………………………………………

Share:

KISA CHA SUNGURA NA MBWEHA

Hapo zamani za kale Sungura walianzisha vita na Tai. Mapambano yalianza na kila upande ukijigamba na kudhani ulikuwa na uwezo wa kumshinda mwenzie.

Vita vilipopamba moto, Sungura walihisi kuzidiwa. Baada ya vikao na mashauriano ya majemedari, walikubaliana kutuma maombi kwa Mbweha ili waje kama mamluki kuwasaidia kupambana na jeshi shupavu la Tai.

Mbweha wakajibu, “tungeweza kuja kuwasaidia kwa moyo mmoja, iwapo tusingeliwafahamu ninyi ni nani, na ni nani hao mnaopigana nao vita.”

Hadithi hii inatufundisha nini?
1……………………………………………………………………………………………………………………
2……………………………………………………………………………………………………………………
3……………………………………………………………………………………………………………………
Taja methali, nahau au msemo wa Kiswahili wenye maana inayofanana na maudhui ya hadithi hii;
………………………………………………………………………………………………………………………
………………………………………………………………………………………………………………………

Share:

KISA CHA MAJOGOO WAWILI NA MWEWE

Majogoo wawili walioishi kwenye zizi moja walianza kupigana wakigombea ukuu katika himaya yao. Mwishowe jogoo Mwekundu alimshinda jogoo Mweupe, ambaye alisalimu amri na kukimbia.
Jogoo Mweupe alienda kujificha kwenye kona ya mbali kwa unyonge, ilhali yule Mwekundu aliyeshinda alirukia juu ya ukuta, akapiga mbawa zake na kuwika kwa sauti kuu kama ishara ya kuwa yeye ndiye mkuu hakuna mwingine zaidi yake. Ghafla Mwewe aliyekuwa akipita juu alimwona akamkamata na kumbeba kwa makucha yake akaondoka naye.
Ndipo yule jogoo Mweupe aliyeshindwa na kujificha alitoka konani na kutawala zizi akiwa huru asiye na mpinzani.

Hadithi hii inatufundisha nini?
1……………………………………………………………………………………………………………………
2……………………………………………………………………………………………………………………
3……………………………………………………………………………………………………………………
Taja methali, nahau au msemo wa Kiswahili wenye maana inayofanana na maudhui ya hadithi hii;
………………………………………………………………………………………………………………………
………………………………………………………………………………………………………………………

Share:

KISA CHA CHURA MTABIBU

Hapo zamani za kale kulikuwako Chura mkubwa.
Siku moja Chura huyo alijitokeza toka nyumbani kwake Kidimbwini Maguguni na kuwatangazia wanyama wote kwa kujitapa kwamba yeye ni mtabibu mjuzi, na ni mbobevu katika masuala ya tiba na dawa. Akatembea kifua mbele na kujigamba kuwa ana uwezo wa kutibu magonjwa ya aina zote, kwa jamii zote za wanyama!

Mbweha alijitokeza na kumuuliza, “Unathubutu vipi kujifanya tabibu wa wengine, ilhali unashindwa kujitibu mwenyewe ulemavu wako wa mwendo na makunyanzi ya ngozi!?”

Hadithi hii inatufundisha nini?
1……………………………………………………………………………………………………………………
2……………………………………………………………………………………………………………………
3…………………………………………………………
Taja methali, nahau au msemo wa Kiswahili wenye maana inayofanana na maudhui ya hadithi hii;
………………………………………………………………………………………………………………………
………………………………………………………………………………………………………………………

Share:

KISA CHA POPO, NDEGE NA WANYAMA

Hapo zamani za kale kulitokea mgogoro mkubwa sana kati ya Ndege na Wanyama, na vita kati yao ilinukia. Ilionekana kana kwamba juhudi zote za mapatano ziligonga mwamba. Wakati majeshi hayo mawili yakijikusanya kujiandaa kwa mapigano ya umwagaji damu, Popo alisita kuchagua upande wa kujiunga nao kivita.
Jeshi la Ndege lilipita karibu na kitulio chake na kumwambia; “Twende nasi vitani ee Popo ndege mwenzetu.”
Popo alikataa na kusema, “Mimi ni mnyama. Wala si ndege kama ninyi”
Baadaye jeshi la Wanyama nalo lilipita chini ya kitulio chake, walipomwona walimwita na kumwambia; “Twende nasi vitani ee Popo myama mwenzetu.” Popo alikataa tena na kujibu, “Mimi ni Ndege. Wala si mnyama kama ninyi.”
Basi kukawa na ngurumo za kutisha za wanyama shupavu kama vile simba duma na tembo; na ndege shupavu kama tai na furukombe. Anga lote lilijaa vitisho na harufu ya damu. Majike wenye ndama na majike wenye makinda walihisi kiyama chao kimefika.
Kwa bahati sana, katika dakika za mwisho mwisho kuelekea vita, muafaka ulifikiwa kati ya pande mbili hizo na vita vikaepukwa. Kukawa na amani badala ya mapigano. Kuona hivyo, Popo naye alitamani kuwa sehemu ya shamrashamra hizo. Alikwenda kwa Ndege akitaka kujiunga nao katika furaha na cherekochereko za kushangilia amani, wakamfukuza.
Akaamua kuondoka akaenda kwa wanyama huku akitabasamu na kutegemea kushiriki nao furaha ile ya amani. Nao walimfukuza kwa hasira hata akalazimika kukimbia wasije wakamdhuru kwa kumjeruhi au kumtoa roho kabisa.
Ah,” Popo alijisemea kimoyomoyo, “sasa nimeng’amua,”

Hadithi hii inatufundisha nini?
1……………………………………………………………………………………………………………………
2……………………………………………………………………………………………………………………
3……………………………………………………………………………………………………………………
Taja methali, nahau au msemo wa Kiswahili wenye maana inayofanana na maudhui ya hadithi hii;
………………………………………………………………………………………………………………………
………………………………………………………………………………………………………………………


Share:

KISA CHA KIJANA MWINDA SENENE

Kijana mmoja mdogo alikuwa akidaka Senene kwenye majani yaliyomea kando ya shamba lao. Ilikuwa ni mapema wakati wa asubuhi, hata umande ungali haujavukizwa. Baada ya nusu saa tu alifanikiwa kuwadaka Senene wengi sana. Wakati akijiandaa kurudi nyumbani, alitupa macho huku na huko na kumwona Nge akiwa amejipachika katikati ya majani mawili. Basi yule Kijana kwa haraka yake hakuweza kutambua kuwa yule ni Nge na badala yake alimfananisha na Senene. Akanyoosha mkono wake ili amkamate, aongezee idadi ya kitoweo.

Nge naye akaunyoosha mwiba wake tayari kwa kung’ata na kumuasa yule Kijana, akasema;
ee Kijana mwenye uchu na ulafi, laiti ungelithubutu hata kunigusa tu, ungejuta, kwani ungelinikosa mimi na pia hao Senene wote uliokwisha kuwapata!”
Share:

KISA CHA SUNGURA NA VYURA

Sungura walikuwa wakionewa sana na wanyama wengine kwa kupigwa, kuwindwa na kuliwa, kiasi kwamba hawakujua wakimbilie wapi. Ikawa wanaishi maisha ya karaha mno na kila walipomwona mnyama yeyote akiwakaribia, walilazimika kutimua mbio kwa woga.
Siku moja wakaliona kundi la Farasi pori walio katika hali ya taharuki wakikimbia na kuwaelekea wao. Walihamaki na kutimka kuelekea ziwani, wakiwa na nia ya kujitupa majini ili wafe, kwani waliona ni heri kufa kuliko kuendelea kuishi katika adha na karaha ile ya kunyanyaswa, na maisha ya roho mkononi.

Lakini walipokaribia kingo za ziwa, kundi la Chura waliokuwa wamejipumzisha wakitafakari, walishtushwa sana na vishindo vya Sungura hao, nao walitaharuki wakageuka kwa woga na kujitupa ziwani kuokoa maisha yao.
Kwa kweli,” alisema mmoja wa Sungura, “kumbe hali yetu sisi siyo mbaya sana kama tunavyodhani.”
Share:

KISA CHA SIMBA NA PAPA

Siku moja Simba alikuwa akirandaranda ufukweni mwa bahari, akamwona Papa akichomoza kichwa chake juu ya uso wa bahari katikati ya mawimbi. Alizama na kuibuka tena… akazama na kuibuka tena… Simba alivutiwa naye na kumwona kuwa anafaa kuwa rafiki kwani ni mkubwa na mwenye nguvu kama yeye.

Alimwita karibu naye akasogea.
Baada ya kusalimiana Simba akamshauri mwenzake kuwa ipo haja ya kufanya makubaliano ya ushirikiano na urafiki baina yao, akimchagiza kuwa kati ya wanyama wote wa mwituni, wao Simba na Papa ndiyo wapaswao kuwa maswahiba haswa. Kwani mmoja wao ni mfalme wa wanyama wote wa nchi kavu ilhali mwingine ni mtawala wa viumbe wote wa baharini.

Papa alilipokea wazo hilo la Simba kwa mikono miwili. Wakakubaliana.
Punde akatokea Mbogo, na Simba, kwa kuwa alikuwa na njaa alimtamani na kuanza kupambana naye. Simba alipoona analemewa aliamwita rafikiye Papa aje nchi kavu kumsaidia.
Papa, ingawa alikuwa na nia ya dhati ya kumsaidia, hakuweza kufanya hivyo kwani hakuwa na namna yoyote ya kuweza kutoka majini.

Simba akamshutumu na kumdhihaki Papa kuwa ni muasi na asiye mwaminifu.
Papa akamjibu; “Hapana rafiki yangu, wala sistahili mzigo huo wa lawama toka kwako, yakupasa umlaumu muumba, ambaye, pamoja na kunipa ukuu na utawala majini, ameninyima kabisa uwezo wa kuishi juu ya nchi kavu.”
Share:

KISA CHA MBWEHA NA MBU

Siku moja, baada ya kutembea kwa muda mrefu, Mbweha aliukuta mto mdogo wenye kina kifupi cha maji. Maji yalikuwa masafi na maangavu kabisa na mandhari ya bonde lile kwa ujumla ilikuwa ya kuvutia kutokana na uoto na magugu yaliyonawiri vizuri pembezoni. Akayatamani maji kwa uzuri wake japo hakuwa na kiu kabla, akayanywa, kisha akatulia kidogo kwa tafakuri.

Hapohapo akapata wazo la kwenda ng’ambo ya mto kumtembelea rafiki yake ambaye hawakuwahi kuonana kwa takribani miezi kenda. Na kwa kuwa ilikuwa muda wa jioni aliona ni vyema zaidi kwani katika mila za kimbweha, kulala kwa rafiki huchukuliwa kama heshima kubwa na ishara ya urafiki wa kweli. Akajitoma majini na kuvuka.
 
Baada ya kufika ng’ambo ya mto Mbweha alijikuta akiunasisha mkia wake kwenye magugu kizembe, na kila alivyofanya jitihada za kujinasua ndo kwanza alijinasisha zaidi. Mwisho akawa hana uwezo wa kwenda wala kusogea.
Kundi la Mbu lilipita eneo lile na kuona tatizo lililomkabili, wakashauriana na kutua wote kwa pamoja kwenye mwili wake, wakamnyonya na kujipatia mlo wa damu pasipo bughudha ya mkia wake.

Nungunungu, akiwa hana hili wala lile, naye akapita mahali pale na kuona matatizo mawili yanayomkabili Mbweha. Alimhurumia sana, akamfuata na kumwambia: “Pole ee jirani yangu, naona upo kwenye mapitio mabaya, je nikusaidie kupunguza maswaibu yako kwa kuwafukuza hao Mbu wakunyonyao damu yako?”
Mbweha aliguna na kumjibu,

Asante sana kwa kunijali na kwa nia yako ya kutaka kunitatulia tatizo moja kati ya mawili haya, rafiki Nungunungu,” alisema, “ila naona ni heri usiwafukuze hawa Mbu.”
Kwa nini, wanakutesa na kukunyonya halafu hutaki niwaondoe!?”
Sikiliza rafiki,” alijibu Mbweha, “Mbu hawa wameninyonya sana na kwa sasa wamekwishashiba, matumbo yao yamejaa damu yangu; endapo utawafukuza hawa, Mbu wengine wenye njaa kali watakuja kuchukua nafasi yao, waninyonye upya na pengine kuniua kabisa.”
ibot.isk@gmail.com  
Share:

KISA CHA SUNGURA NA MBWA

Katika pitapita zake za mawindo, Mbwa alimvumbua Sungura kwenye maficho yake. Akaanza kumkimbiza. Baada ya kukimbizana kwa muda mrefu, Mbwa alishindwa kumkamata kutokana na Sungura kumpiga chenga lukuki za maudhi. Akaamua kusimama.

Kundi la Mbuzi lilikuwapo mahali pale na walishuhudia kinagaubaga sakata hilo. Ikawa burudani kwao kwani mioyoni walikuwa wakimshabikia Sungura, na hawakupenda akamatwe na kuuawa. Walipomwona Mbwa akisimama kabla ya kutimiza azma yake ya kumkamata Sungura walimcheka na kumdhihaki sana,
wakimwambia “yule Sungura mdogo ndiye mkimbiaji hodari kuliko wewe Mbwa mkubwa!?”
Mbwa akawajibu, “shida ni kuwa hamjang’amua tofauti kati yetu: Mie nilikuwa nikikimbia ili tu nipate mlo wa jioni, wakati yeye alikimbia ili aokoe maisha yake.”
Share:

KISA CHA MBUZI NA MCHUNGAJI

Mchunga Mbuzi alihangaika kumrudisha Mbuzi mmoja aliyetoka kundini na kuingia kwenye shamba la jirani. Alipiga mbinja na kupuliza baragumu bila ya mafanikio; yule Mbuzi alimbeza na kuidharau miito yote. Mwishowe Mchunga Mbuzi aliudhika na kumrushia jiwe kwa nguvu, likamvunja pembe moja.

Kuona vile Mchunga Mbuzi alipagawa kwa huruma na hofu. Alimbembeleza yule Mbuzi kwamba watakaporejea nyumbani asimdondolee bwana mwenye mbuzi kilichosibu. Mbuzi akamjibu, “Kivipi ewe Mchunga mpumbavu, hujui kuwa hata nikifunga mdomo wangu, pembe yenyewe itaongea!”
Share:

KISA CHA BABU KIZEE NA KIFO

Babu kizee mmoja aliajiriwa kufanya kazi ya kukata magogo ya miti msituni. Siku moja akiwa anarejea nyumbani jioni alibebeshwa mzigo wa kuni aupeleke mjini ukauzwe. Mzigo ule ulikuwa mzito sana kwake.
Baada ya mwendo wa kitambo kirefu alichoka akawa hoi kabisa. Alisononeka kwa ufukara wake unaopelekea apate mateso ya kufanya kazi mzito mchana kutwa, na jioni kutwikwa mizigo mizito katika umri kama ule.
Mwishowe aliamua kuutupa chini mzigo ule, akaketi kando ya njia, akajiinamia na kuomba kwa dhati kabisa “Kifo” kimchukue aepuke suluba na mateso ya kubeba mzigo ule.
Kwa bahati nzuri ombi lake lilisikika na kutekelezwa bila ucheleweshaji; alipoinua uso wake baada ya kumaliza kuomba, alimwona “Kifo” amesimama mbele yake tayari kwa kazi, akiwa amekuja kuitika ule wito wake.
Kifo akauliza, “nimesikia wito wako ee mzee, je unataka nini hata ukaniita nikujie?”
Mzee akajibu haraka, “nilihitaji unipe msaada wa kuuinua mzigo huu wa kuni, unitwike mabegani kwangu niendelee na safari.”
Share:

KISA CHA AYALA NA MZABIBU

Ayala, baada ya kukimbizwa na kuandamwa na wawindaji toka mbali, alichoka sana na kujua sasa mwisho wake umefika. Wawindaji walipomkaribia alifanya hila, akachupa kuume na kujibanza kwenye mvungu wa majani makubwa ya
Mzabibu. Wawindani nao kwa haraka waliyokuwa nayo (na hulka ya kuwahi ni kupata) hawakuweza kuing’amua hila yake, wakampita palepale bila kumwona.
Baada ya muda mfupi, kwa kudhani kuwa hatari haipo tena, Ayala aliinuka na kuanza kuyanyofoa nyofoa yale majani ya Mzabibu. Mwindaji mmoja aliyekuwa nyuma ya wenzake alisikia kwa mbali ule mchakato wa majani, akageuka kuangalia nyuma walikotoka, akamwona yule Ayala chini ya Mzabibu. Akachomoa mshale, akauweka kwenye upinde, akapiga na kumchoma Ayala tumboni.
Ayala, wakati akitapatapa karibia kukata roho, alikoroma na kusema; “Nimepata tijara nistahiliyo, kwani sikupaswa kabisa kuyatendea vile majani ya Mzabibu ambao punde uliokoa maisha yangu.”
Share:

KISA CHA MAKSAI NA WACHINJA NG'OMBE

Maksai, hapo zamani za kale, waliazimia kufanya hila ya kuwashambulia ghafla na kuwaangamiza Wachinja ng’ombe wote, kwa kuwa walikuwa wanaendesha biashara inayoteketeza jamii yao. Azimio hilo lilipitishwa kwa wingi mkubwa wa kura na maandalizi ya utekelezaji wake yakaanza mara moja.
Siku ya siku ilipofika walikusanyika ili waweze kutekeleza azma hiyo ya mauaji ya kushtukiza. Walinoa pembe zao vizuri kujiandaa kwa mapambano. Hamasa ilikuwa kubwa, na vijana walichagizwa kukaa mstari wa mbele.
Lakini miongoni mwao kulikuwako Maksai mmoja ambaye alikuwa mzee sana kwa umri (na wingi wa mashamba aliyokwishalima katika maisha yake) akawaasa kwa kuwaambia: “Ni kweli, Wachinja ng’ombe hawa wanatuchinja na kutuua, lakini tusisahau kuwa wanafanya hivyo kwa ujuzi na taaluma ya hali ya juu, na hivyo hutuepusha na maumivu yasiyo ya lazima. Endapo tutawashambulia na kuwaangamiza, tutaangukia mikononi mwa wafanyabiashara wasio na ujuzi wa kuchinja, na tutaanza kuuawa kwa nyundo na mashoka, kwa mateso na maumivu makali. Itakuwa ni kifo mara mbili zaidi: kwani hakika nawaambieni, ingawa tutawaangamiza Wachinja Ng’ombe wote, bado binadamu wataendelea kuhitaji nyama ya ng’ombe daima.”
Share:

Jumamosi, 21 Desemba 2013

KISA CHA MJAKAZI NA NYOKA

Hapo zamani za kale, kulikuwapo Nyoka mkubwa mwenye sumu kali, ambaye aliweka makazi yake kwenye shimo pembezoni mwa baraza ya nyumba ya Mjakazi mmoja. Siku moja usiku wa manane yule Nyoka alimng’ata mtoto mchanga wa Mjakazi, mwili wake ukabadilika rangi kuwa mweusi tii, akafa.
Kukawa msiba na simanzi isiyo kifani.
Wakati akiomboleza kifo cha mwanae kwa uchungu, mtu huyo aliapa kulipiza kisasi kwa kumuua Nyoka huyo pindi atakapopata wasaa.
Siku iliyofuata, majira ya jioni, Nyoka yule alitoka shimoni ili kwenda kujitafutia chakula. Ndipo Mjakazi alimwona akitambaa kwenye kiambaza kuelekea ndani, akachukua shoka na kumwendea kwa hasira ili ammalize. Na kwa kuwa
alinyanyua shoka na kutaka kumshambulia kwa papara, alikikosa kichwa na kiwiliwili na badala yake akamkata ncha ya mkia tu.
Nyoka akafanikiwa kujiokoa na kurudi ndani ya shimo.
Baada ya siku kadhaa kupita, Mjakazi yule akalemewa na hofu ya kuwa yeye pia yu hatarini kung’atwa na yule Nyoka. Akapata wazo la kuanzisha mchakato wa kumrubuni nyoka waafikiane kuishi kwa amani. Akamtengea mikate na chumvi kando ya shimo lake, na maji ya kunywa, ikiwa ni ishara ya kuomba urafiki.
Yule nyoka, huku akitoa mlio wa tahadhari na kitisho, alimwambia: “ndugu, kamwe hakuwezi kuwa na amani ya kweli kati yako nami; kwani kila nitakapokuona nitakumbuka nilivyopoteza mkia wangu, nawe kila unionapo utakumbuka kifo cha mwanao.”
Share:

KISA CHA NGURUWE, KONDOO NA MBUZI

Nguruwe mmoja mdogo alikuwa amefungiwa kwenye uzio wa miti. Mbuzi na Kondoo pia walifungwa pamoja naye. Siku moja Mchungaji wao alikuja na kumkamata yule Nguruwe, ambaye aliguna na kuanza kupiga kelele na kufurukuta.
Mbuzi na Kondoo walimlalamikia Nguruwe kwa kelele zake za kilio na purukushani, wakasema kwa kejeli, “Mara kwa mara Mchungaji wetu hutushika sisi, na hatuangui kilio kama yeye.”
Kusikia hivyo, Nguruwe akawajibu, “Mchungaji anavyowashika ninyi na anavyonishika mimi ni vitu viwili tofauti kabisa. Kwani anapowashika ninyi huhitaji kutoka kwenu sufu na maziwa tu, lakini anaponishika mimi ana nia ya kunipokonya uhai wangu.”
Hadithi hii inatufundisha nini?
 
Taja methali, nahau au msemo wa Kiswahili wenye maana inayofanana na maudhui ya hadithi hii;


Share:

KISA CHA MVUVI NA SAMAKI MDOGO

Ilitokea siku moja kuwa, Mvuvi, baada ya kuhangaika kwenye kazi yake ya kuvua kutwa nzima, aliambulia kukamata Samaki mmoja tu mdogo.
Yule Samaki akamwambia Mvuvi kwa kumbembeleza;
Tafadhali niachie ee bwana,” alilalamika. “Mimi bado ni mdogo sana, sijafikia rika ya kuliwa nawe kwa sasa. Ukinihurumia na kunirudisha mtoni, nitakua haraka, na ndipo baadaye utanivua na nitafaa sana kwa kitoweo wakati huo.”
AAh!, hapana, hapana ee Samaki mdogo,” alisema Mvuvi, “Nimekupata sasa. Huenda nisikupate tena baadaye.”
Share:

KISA CHA MWANAKONDOO NA MBWA MWITU

Mbwa mwitu alimkimbiza Mwanakondoo, ambaye ili kujiokoa alikimbilia ndani ya hekalu moja la ibada. Mbwa mwitu hakuweza kuingia hekaluni, badala yake alisimama nje akapaza sauti kumwita akimwambia, “Ni heri uje kwangu, maana humo ulimokimbilia Padre akikukamata atakuchinja na kukufanya dhabihu.”
Mwanakondoo akamjibu, “Ni heri nitolewe kafara ndani ya hekalu la Mungu kuliko kuja kwako nikaliwa nawe.”

Share:

Live Traffic Feed

Blogroll

BTemplates.com

Inaendeshwa na Blogger.

Jumla ya Mara Iliyotazamwa

Popular Posts

Kumbukumbu la Blogu