Babu kizee
mmoja aliajiriwa kufanya kazi ya kukata magogo ya miti msituni. Siku
moja akiwa anarejea nyumbani jioni alibebeshwa mzigo wa kuni aupeleke
mjini ukauzwe. Mzigo ule ulikuwa mzito sana kwake.
Baada ya
mwendo wa kitambo kirefu alichoka akawa hoi kabisa. Alisononeka kwa
ufukara wake unaopelekea apate mateso ya kufanya kazi mzito mchana
kutwa, na jioni kutwikwa mizigo mizito katika umri kama ule.
Mwishowe
aliamua kuutupa chini mzigo ule, akaketi kando ya njia, akajiinamia
na kuomba kwa dhati kabisa “Kifo” kimchukue aepuke suluba na
mateso ya kubeba mzigo ule.
Kwa bahati
nzuri ombi lake lilisikika na kutekelezwa bila ucheleweshaji;
alipoinua uso wake baada ya kumaliza kuomba, alimwona “Kifo”
amesimama mbele yake tayari kwa kazi, akiwa amekuja kuitika ule
wito wake.
Kifo
akauliza, “nimesikia wito wako ee mzee, je unataka nini hata
ukaniita nikujie?”
Mzee akajibu haraka, “nilihitaji unipe msaada wa
kuuinua mzigo huu wa kuni, unitwike mabegani kwangu niendelee na
safari.”
0 maoni:
Chapisha Maoni