Hapo zamani
za kale, kulikuwapo Nyoka mkubwa mwenye sumu kali, ambaye aliweka
makazi yake kwenye shimo pembezoni mwa baraza ya nyumba ya Mjakazi
mmoja. Siku moja usiku wa manane yule Nyoka alimng’ata mtoto
mchanga wa Mjakazi, mwili wake ukabadilika rangi kuwa mweusi tii,
akafa.
Kukawa msiba
na simanzi isiyo kifani.
Wakati
akiomboleza kifo cha mwanae kwa uchungu, mtu huyo aliapa kulipiza
kisasi kwa kumuua Nyoka huyo pindi atakapopata wasaa.
Siku
iliyofuata, majira ya jioni, Nyoka yule alitoka shimoni ili kwenda
kujitafutia chakula. Ndipo Mjakazi alimwona akitambaa kwenye kiambaza
kuelekea ndani, akachukua shoka na kumwendea kwa hasira ili ammalize.
Na kwa kuwa
alinyanyua
shoka na kutaka kumshambulia kwa papara, alikikosa kichwa na
kiwiliwili na badala yake akamkata ncha ya mkia tu.
Nyoka
akafanikiwa kujiokoa na kurudi ndani ya shimo.
Baada ya siku
kadhaa kupita, Mjakazi yule akalemewa na hofu ya kuwa yeye pia yu
hatarini kung’atwa na yule Nyoka. Akapata wazo la kuanzisha
mchakato wa kumrubuni nyoka waafikiane kuishi kwa amani. Akamtengea
mikate na chumvi kando ya shimo lake, na maji ya kunywa, ikiwa ni
ishara ya kuomba urafiki.
Yule nyoka, huku akitoa mlio wa tahadhari na kitisho,
alimwambia: “ndugu, kamwe hakuwezi kuwa na amani ya kweli kati yako
nami; kwani kila nitakapokuona nitakumbuka nilivyopoteza mkia wangu,
nawe kila unionapo utakumbuka kifo cha mwanao.”
0 maoni:
Chapisha Maoni