Hadithi za kale zenye mafundisho za Esopo zilizoandikwa zaidi ya miaka 3000 iliyopita. Zimetafsiriwa kwa Kiswahili na Issa S. Kanguni, chini ya shirika lisilo la kiserikali la Tanzania Inventors and Techno-Thinkers Consortium (TITC). Tel; +255757242960

Tafuta katika Blogu Hii

Pages

Alhamisi, 1 Machi 2018

Mbweha na Beberu



Siku moja Mbweha alitumbukia kisimani kwa bahati mbaya, na ingawa kisima chenyewe hakikuwa na kina kirefu sana, alijikuta akishindwa kutoka nje tena. Baada ya kuhangaika kwa muda mrefu bila mafanikio, hatimaye akatokea Beberu mwenye kiu kali. Beberu alidhani kuwa Mbweha ametumbukia kwenda kunywa maji kukidhi kiu yake, na hivyo akauliza kama maji yalikuwa safi au la.

“Ni safi na matamu kupita maji yote kwenye nchi hii,” alijibu Mbweha yule mjanja, “jirushe utumbukie ujionee mwenyewe. Maji ni mengi yanatutosha sote na tutasaza.”

Beberu mwenye kiu mara moja alijitosa kisimani na kuanza kuyafakami maji. Mbweha naye kwa haraka sana alimdandia Beberu mgongoni akachupa kwenye ncha za pembe za Beberu na kutoka zake nje ya kisima.
Yule Beberu mpumbavu akang’amua kuwa amejiingiza matatizoni, akaanza kumbembeleza Mbweha amsaidie kumtoa kisimani. Lakini Mbweha tayari alikwishaanza kutokomea zake mitini.

“Laiti ungalikuwa na akili kama ulivyo na ndevu, rafiki,” alimwambia huku akikimbia zake, “ungalikuwa makini na kujaribu kung’amua kwanza njia utakayoitumia kutokea kisimani kabla hujatumbukia.”

Mwisho.
Share:

Jumatano, 28 Februari 2018

Kisa cha Beberu Wawili

    Mbuzi wawili Beberu walikuwa wakirandaranda kwenye pande mbili za mlima kila mmoja kivyake. Kwa bahati mbaya walikutana kwenye eneo lenye korongo lenye kina kirefu sana ambalo chini yake kulikuwa na mto mkubwa uliotiririka kwa kasi.
    Tawi la mti ulioanguka lilikatiza juu ya korongo hilo na ndo lilikuwa njia pekee ya kuweza kuvuka, na juu ya tawi hilo hata panya buku wawili wasingaliweza kupita kwa pamoja salama. Kwa jinsi njia hiyo ilivyokuwa nyembamba kulinganisha na ukubwa wa korongo, hata kiumbe jasiri vipi angalitetemeka kwa woga.
    Lakini si kwa Beberu wale. Kwa tabia yao ya kiburi na kupenda kujikweza, hakuna mmoja kati yao aliyekuwa tayari kumpisha mwenzie avuke kwanza.
    Basi ikawa, Beberu mmoja alikita miguu kibabe kwenye gogo. Na mwingine naye akafanya vivyo hivyo. Katikati waliinamisha vichwa wakaumanisha pembe zao. Hivyo walianza kusukumana na hatimaye wote walianguka korongoni wakasombwa na maji na kuangamia.

Mwisho
Share:

Live Traffic Feed

Blogroll

BTemplates.com

Inaendeshwa na Blogger.

Jumla ya Mara Iliyotazamwa

Popular Posts

Kumbukumbu la Blogu