Siku moja,
baada ya kutembea kwa muda mrefu, Mbweha aliukuta mto mdogo wenye
kina kifupi cha maji. Maji yalikuwa masafi na maangavu kabisa na
mandhari ya bonde lile kwa ujumla ilikuwa ya kuvutia kutokana na uoto
na magugu yaliyonawiri vizuri pembezoni. Akayatamani maji kwa uzuri
wake japo hakuwa na kiu kabla, akayanywa, kisha akatulia kidogo kwa
tafakuri.
Hapohapo
akapata wazo la kwenda ng’ambo ya mto kumtembelea rafiki yake
ambaye hawakuwahi kuonana kwa takribani miezi kenda. Na kwa kuwa
ilikuwa muda wa jioni aliona ni vyema zaidi kwani katika mila za
kimbweha, kulala kwa rafiki huchukuliwa kama heshima kubwa na ishara
ya urafiki wa kweli. Akajitoma majini na kuvuka.
Baada ya
kufika ng’ambo ya mto Mbweha alijikuta akiunasisha mkia wake kwenye
magugu kizembe, na kila alivyofanya jitihada za kujinasua ndo kwanza
alijinasisha zaidi. Mwisho akawa hana uwezo wa kwenda wala kusogea.
Kundi la Mbu
lilipita eneo lile na kuona tatizo lililomkabili, wakashauriana na
kutua wote kwa pamoja kwenye mwili wake, wakamnyonya na kujipatia mlo
wa damu pasipo bughudha ya mkia wake.
Nungunungu,
akiwa hana hili wala lile, naye akapita mahali pale na kuona matatizo
mawili yanayomkabili Mbweha. Alimhurumia sana, akamfuata na
kumwambia: “Pole ee jirani yangu, naona upo kwenye mapitio mabaya,
je nikusaidie kupunguza maswaibu yako kwa kuwafukuza hao Mbu
wakunyonyao damu yako?”
Mbweha
aliguna na kumjibu,
“Asante
sana kwa kunijali na kwa nia yako ya kutaka kunitatulia tatizo moja
kati ya mawili haya, rafiki Nungunungu,” alisema, “ila naona ni
heri usiwafukuze hawa Mbu.”
“Kwa nini,
wanakutesa na kukunyonya halafu hutaki niwaondoe!?”
“Sikiliza rafiki,” alijibu Mbweha, “Mbu hawa
wameninyonya sana na kwa sasa wamekwishashiba, matumbo yao yamejaa
damu yangu; endapo utawafukuza hawa, Mbu wengine wenye njaa kali
watakuja kuchukua nafasi yao, waninyonye upya na pengine kuniua
kabisa.”
ibot.isk@gmail.com
0 maoni:
Chapisha Maoni