Hadithi za kale zenye mafundisho za Esopo zilizoandikwa zaidi ya miaka 3000 iliyopita. Zimetafsiriwa kwa Kiswahili na Issa S. Kanguni, chini ya shirika lisilo la kiserikali la Tanzania Inventors and Techno-Thinkers Consortium (TITC). Tel; +255757242960

Tafuta katika Blogu Hii

Pages

Jumatano, 30 Aprili 2014

MIFUKO YA DHAMBI

Kwa mujibu wa masimulio ya ngano za kale za mababu zetu, eti inasemekana kwamba kila binadamu hapa duniani amezaliwa na mifuko miwili ikining'inia shingoni mwake. 

Fuko kubwa la mbele linajazwa mapungufu na madhambi ya majirani zake, na fuko kubwa linaloning'inia nyuma linajazwa mapungufu na madhambi yake mwenyewe.

 Ndiyo maana watu ni wepesi kuona na kulaumu makosa ya wenzao, huku mara nyingi wakishindwa kutambua mapungufu yao wenyewe.
***
Share:

KISA CHA MWINDAJI NA MVUVI

Mwindaji, akiwa na mbwa wake anarejea kutoka mawindoni, kwa bahati alikutana na Mvuvi ambaye naye alikuwa anarejea nyumbani toka ziwani na kapu lake lililojaa samaki. 

Basi ikawa yule Mwindaji akatamani sana wale samaki kwenye kapu la Mvuvi, ilhali yule Mvuvi naye alitamani sana kitoweo kilichopo kwenye mkoba wa yule Mwindaji.

Kwa hiyo mara moja wakakubaliana kubadilishana mawindo yao ya siku kwa Mvuvi kuchukua mkoba wa Mwindaji na Mwindaji kuchukua fuko la samaki. Kila mmoja alifurahia sana makubaliano yale kiasi cha kwamba waliendelea kufanya vile siku hadi siku.
 
Mwishowe jirani yao mmoja akawaambia, "Enyi wandugu, iwapo mtaendelea kwa mwenendo huu, muda si mrefu mtaharibu raha ya kubadilishana kwa kuwa mnabadilishana kila siku, na hatimaye kila mmoja wenu atapenda abaki na chake."
***
Share:

KISA CHA MPIGA-TARUMBETA VITANI

Hapo zamani za kale, kulikuwapo bwana mmoja mpiga tarumbeta ambaye alikuwa jasiri akiwaongoza askari  vitani. 

Basi siku moja huku vita ikiwa imepamba moto, alisogea kuwakaribia maadui kupita kiasi, matokeo yake akakamatwa. Wakati wakijiandaa kumnyonga, akaanza kulia na kubembeleza asiuawe na badala yake aachiwe huru, "Tafadhalini niacheni, msiniue nihurumieni kwa kuwa mimi sina hatia" akasema "mimi si mpiganaji, sijaua mtu yeyote, na sina hata silaha. Mi napiga tu tarumbeta hili, na kwa kweli sidhani kama hiyo inamuumiza yeyote kati yenu. Sioni sababu ya nyie kunidhuru!"

"Ingwa haupambani mwenyewe" wakamjibu "lakini unapopiga tarumbeta lako unawahimiza na kuwaongoza watu wako kupambana nasi. Na hiyo ni sababu tosha kukuadhibu."
Share:

Jumapili, 27 Aprili 2014

KISA CHA WEZI NA JOGOO

Vibaka walivunja nyumba ili wakaibe na walipoingia ndani hawakukuta kitu chochote isipokuwa jogoo. Wakamkamata jogoo yule na kuondoka naye haraka. 

Walipofika kwao walijiandaa kumchinja jogoo watengeneze kitoweo, ambapo jogoo alianza kujitetea asiuawe: “Tafadhalini msinichinje; ni vyema mkanifuga kwani ninasaidia sana watu. Ninawaamsha watu usiku ili wawahi makazini kwao.”

 “Hiyo ndiyo sababu mojawapo inayotufanya lazima tukuchinje” wakamjibu “kwani kila unapowaamsha majirani zako, unatuharibia sisi na unakatisha muda wetu wa kazi.”
***


Share:

KISA CHA KIBAKA NA MAMAYE

Hapo zamani za kale kulikuwepo mvulana mmoja aliyeishi na mama yake. Siku moja, akiwa shuleni kijana aliiba kitabu cha mwanafunzi mwenzake na kurudi nacho nyumbani akamwonyesha mama yake. Yule mama, sio tu hakumchapa wala kumgombeza, bali alimpongeza. 

Kijana akakua kuelekea utu uzima, huku akiendelea na tabia yake ya wizi wa vitu vikubwa zaidi. 

Wanasema za mwizi arobaini. Mwishowe ilitokea siku akakamatwa akijaribu kutaka kuiba, na akiwa amefungwa mikono yake kwa nyuma na wananchi wenye hasira, akapelekwa kwenye uwanja maalum ambapo wahalifu hupewa adhabu ya kunyongwa hadharani. 

Mama yake naye akafuata msafara akilia na kujipigapiga kwa huzuni na uchungu wa mwanaye, ambapo yule kijana kuona vile akasema, “Naomba kuongea na mama yangu nimnong'oneze jambo tafadhali.” Mama yake akamsogelea kumsikiliza. 
Basi yule kijana alimng'ata sikio kwa nguvu nusura anyofoe kipande.

Mama yake akamfokea na kumtolea maneno ya kumlaani kwamba ni mtoto mbaya, naye akajibu “Ah! Laiti ungalinichapa na kunikemea siku ya kwanza nilipoiba na kukuletea kile kitabu, yasingenifika haya, na wala nisingalikufa kifo cha aibu kama hiki.”

***
Share:

Jumatano, 23 Aprili 2014

NIPE RISITI - La Sivyo...




Onyo; Hadithi hii ni ya kubuni (fiction) na haina uhusiano na tukio lolote lililowahi kutokea. Majina ya wahusika na tabia zao hazina uhusiano na mtu yeyote halisi hivyo ikitokea aina yoyote ya kufanana ni bahati mbaya tu. 

Mtunzi; Issa S. Kanguni
0757242960 /  0655242960
ibot.isk@gmail.com

Haki zote zimehifadhiwa.




Chapter One

          Sauti na kikiri kakara toka chumba cha pili zilimshtua kutoka usingizini. Alitupa shuka kando, akajiviringisha upande na kujiinua kiwiliwili. Akafikicha macho kwa mkono wa kushoto na kushusha miguu chini kabla ya kunyanyuka na kusimama wima huku vifundo vya miguu vikaalika na mapaja yake laini kusisimka. Alipapasa kiberiti awashe kibatari akasita. Akiwa mtupu vilevile bila kujisitiri alitembea kwa kunyata hadi mlangoni kuhakiki kama kweli jana kabla ya kulala aliufunga kwa komeo. Aliporidhika akatembea tena kwa kunyata hadi kwenye kidirisha kidogo upande wa pili wa chumba chake. Akachungulia nje. Bado giza... hakujapambazuka. Nyimbo hafifu za ndege zilizosikika toka mabondeni mbali zilimpa hakika kwamba pambazuko lilikuwa limekaribia. Kiupepo cha ubaridi kilipuliza kuashiria mwanzo wa msimu wa kipupwe.  
          Nia yake ilikuwa ni kuondoka kukiwa bado giza na alijua ana dakika chache tu zakujiandaa na kutoka, vinginevyo mpango mzima ungelivurugika.
          Maandalizi ya kila kitu alishayafanya tangu usiku kabla ya kulala. Giza lilijaribu kumzuia asione, halikufanikiwa.
Alisogea kitandani akafunua godoro mchagoni na kulishikilia kwa mkono wa kushoto huku mkono wa kuume ukipapasa papasa na hatimaye kutoa kitita cha nguo zilizokunjwa vizuri. Harakaharaka akashusha godoro na kuanza kuvaa. Alianza boxer mpya nyeupe yenye urembo wa kung’aa ng’aa na picha ya mkuki moyoni, halafu suruali ya jinsi nyeusi ya kubana, akafunga mkanda. Kisha akavaa sidiria tatu, ya kwanza nzito nyeupe, ya pili nyeupe tena na ya tatu nyeusi. Zilimkaa vyema.  Halafu akaikunjua na kuivaa blauzi ya rangi ya kijivu yenye madoadoa ya pinki na mikunjo shingoni, na baada ya hapo akavaa wigi lenye nywele ndefu kichwani. Alipomaliza, alikuwa na mwonekano wa msichana wa miaka mitana zaidi ya umri wake. Just how she wanted!
“Leo ndio leo…” alijisemea kimyakimya “ama zao ama zangu. Kama wanajifanya wao ndo wanajua mapenzi sasa leo ndo mwisho wao.”
Aliinama akafungua kishubaka cha kitanda na kutoa vifaa vyake vya kazi, kibunda cha pilipili ya unga, nyembe tatu mpya, na kifaa maalum alichokibuni na kukiunda mwenyewe na kukiita kwa kifupi FZ (anatamka efzii), akaviweka kwenye mkoba mweusi pamoja na miwani ya giza, mtandio na kamba ya nailon.
          Alivaa raba, akafunga gidamu. Alisimama akajinyoosha na kujiweka sawa. Aliuweka mkoba begani na kutembea kwa uangalifu hadi mlangoni, akanyoosha mkono ili afungue, mara akasikia mlango wa chumba cha pili unafunguliwa. Akasubiri.
“Hapa leo huendi… kama hutaki twende wote huendi…” sauti ya mwanamke ilisikika ikisema kwa  kulalamika.
“Haya… mdomo si mali yako. Lalama weeee, mwisho wa siku mi siwezi kukatisha safari yangu.” Mwanaume alijibu taratibu kwa dharau.
“Twende sote… kwani kuna tatizo gani tukienda sote?” alihoji mwanamke.
“Kwani n’kienda peke yangu kuna tatizo gani?”
“Kuna tatizo gani!... yaani unauliza kuna tatizo gani? Kwani we hujui? …huendi. La kama uk’enda peke yako basi usichukue pesa zote, chukua nusu.”
“Ili?”
“Ukienda na pesa zote ndo haurudi tena wewe… hadi ziishe..”
“Unaota wewe…” akamsonya “… unajifanya unataka kunilinda mimi utaweza wapi… nipishe huko. Unasahau ni nani kamwoa mwenzie humu ee… sasa kwa taarifa yako… ipo’ivi… kadri unavyozidi kujifanya unanipangia masharti ndo kwanza unazidi kunichefua. Kwa mfano, nilipanga kuacha kiasi cha pesa sasa…” ilisikika sauti ya zipu ikifunguliwa kwa nguvu “…nachukua zote. Funga domo lako. Na umesema sitorudi hadi ziishe… well… omba mungu…”
“Lakini kwa nini mume wangu unanifanyia hivi!... mbona unapokuwa huna pesa tunakaa vizuri… sasa…”
“Aaagh… haukomi tu na mahubiri yako we mwanamke… sasa leo n’takuonyesha… na tena ndo kwanza unasababisha n’ondoke kabla ya mawio. N’mekuchoka… mwanamke gani wewe… sura mbaya na gubu haviendi… afu tena unasahau sheria inaniruhusu kuwa na wangapi.”
“Lakini kumbuka tulikotoka mume wangu.”
“Tulikotoka?... ipo’ivi… sahau tulikotoka. Ndo’ubovu wa uchumba wa kushinikizwa na wazazi… we kwa akili yako unadhani kosa kushinikizwa ni n’ngekuoa wewe na matege kama hayo!? No. na hata kama n’ngekuoa ingelikuwa ni kwa maamuzi yangu mwenyewe si kwa shuruti ya wazazi kisa etu una tabia njema… haya sasa tabia njema i wapi leo...”
Mwanamke alijaribu kusema jambo akashindwa. Akaanza kulia kwa uchungu. Ni dhahiri haikuwa mara yake ya kwanza kusemwa na kutendwa vibaya katika ndoa yake, ila kudharauliwa kulimuuma sana. Na mume wake hakuwa mwepesi wa kuinua mkono kupiga, bali ulimi. Mara zote alilenga kujeruhi moyo, si mwili. Alisikika akijitupa chini na kuanza kulia… kilio cha yaliyopita, yaliyopo, na yajayo.
 Mlango ukabamizwa, sauti ikakoma. Nyayo zilisikika zikipita kwenye ususu kwa haraka kisha mlango wa kutokea nje ukafunguliwa, halafu baadaye ule wa maliwatoni.
Alijua kinachoendelea nje. Alijua anachopaswa kufanya.
          Bila kupoteza muda, hasira zake zikiwa zimeongezeka maradufu, alifungua mlango akatoka na kuufunga nyuma yake. Alipiga hatua ndefu ndefu na kufika kwenye mlango wa nje ambao uliachwa wazi akachungulia nje kwa tahadhari kisha akainama na kutoka taratibu. Sekunde chache baadaye alijikuta uchochoroni nje ya nyumba kukiwa bado na giza. Hasira na chuki dhidi ya baba yake, na huruma na upendo kwa mama yake vilisaidia kumwondoa woga ingawa ilikuwa ndo mara yake ya kwanza kutoka nyumbani kwao katika muda na staili kama ile. Mawingu yalianza kujongea kugubika anga na kufanya giza liwe totoro. Akatafuta sehemu nzuri ya kujibanza kando ya barabara chini ya mti. Sauti kali ya bundi ilisikika ikitokea kwenye moja kati ya miti mitatu mikubwa jirani na pale alipojificha. Hakujali.

          “Leo ndo leo… ama zao ama zangu.” Alijisemea tena kwa sauti yenye hisia kali ya kisasi na kupania. Alifungua pochi kutoa mtandio huku akiangaza kila upande, akajitanda na kuketi kwenye kigingi. Akasubiri…

Itaendelea....


Share:

Jumapili, 20 Aprili 2014

KISA CHA NJIWA MWENYE KIU





Njiwa, akiwa amezidiwa na kiu kupita kiasi, aliona picha ya mtungi wa maji iliyochorwa kwenye bango. 

Basi bila kuangalia kwa makini, aliruka kwa pupa kuulekea mtungi huku akipiga kelele ya shangwe, pasi kujua kuwa ule ni mchoro tu. 

Matokeo yake akajibamiza kwenye bango na kujiumiza vibaya. 

Kwa kuwa alivunjika mbawa zake kwenye mshindo ule, alidondoka chini, na kukamatwa na jamaa mmoja mwenye uchu aliyekuwako kando.
Akafanywa kitoweo.
Share:

KISA CHA BWANA MWENYE WAKE WAWILI






 
Hapo zamani za kale, kulitokea bwana mmoja wa makamo ambaye alikuwa na wake wawili, mmoja mtu mzima na mwingine kijana; ambapo wote walimpenda sana, na kila mmoja alitamani awe anaendana naye. 

Na kwa wakati ule yule bwana nywele zake zilianza kuota mvi, jambo ambalo mke mdogo hakupendezwa  nalo, kwani lilimfanya aonekane ameolewa na mzee asiye makamo yake. 
Basi ikawa kila usiku alichukua chanuo akamchana nywele na kung'oa kila mvi anayofanikiwa kuiona. 

Lakini yule mke mkubwa alifurahi sana kuona mumewe anaota mvi, kwani hakupenda azeeke peke yake kwa maana angeweza hata kufananishwa na mama yake badala ya mke. Basi naye kila asubuhi alimkalisha mumewe na kuanza kumtengeneza nywele, huku akinyofoa nywele nyeusi kidogo kidogo zibaki mvi. 

Matokeo yake, muda si mrefu yule bwana akawa na kipara kabisaa, nywele zote kwisha!

ibot.isk@gmail.com
+255 757 242960  &  +255 655 242960
Share:

Kisa cha Simba Aliyezama Kwenye Mapenzi


Hapo zamani za kale,

Simba, mfalme wa mwitu, alitokea kumpenda binti mzuri wa jamaa mmoja mkata miti. Akapeleka maombi ya kinguvu ya kutaka amwoe. Baba wa binti yule, hakupenda kuruhusu mwanaye aposwe na mfalme Simba, lakini pia aliogopa kukataa ombi hilo. 

Akajikuta njiapanda, asijue akatae au akubali.
Hivyo ikamlazimu atumie mbinu kujinasua kwenye maswahibu hayo. 
Akamwambia mfalme Simba kwamba yeye yupo tayari kumwozesha binti yake, ila kwa sharti moja kuu: kwamba ataridhia ndoa hiyo iwapo ataruhusiwa kumng'oa Simba meno yake pamoja na kumkata makucha, akidai kuwa binti yake anaogopa sana vitu hivyo. 

Mfalme Simba kwa furaha akaafiki sharti hilo.

Basi ikawa siku aliporudi kwenda kuposa akiwa hana meno wala makucha, yule mkatamiti, akawa hamwogopi tena, akamtimua kwa marungu, na Simba akakimbia zake vichakani asirudi tena!
Share:

Live Traffic Feed

Blogroll

BTemplates.com

Inaendeshwa na Blogger.

Jumla ya Mara Iliyotazamwa

Popular Posts

Kumbukumbu la Blogu