Panya Pori alimwalika panya wa mjini, ambaye ni
rafiki yake kipenzi, amtembelee kwake aje ajionee maisha ya porini. Wakiwa kwenye
uwanda wazi wa mashamba, wakila mabaki ya nafaka na mizizi ya miti iliyong’oka,
Panya wa Mjini alimwambia rafiki yake,
“Huku shamba rafiki yangu unaishi maisha ya
wadudu, yaani kama mchwa ama sisimizi, wakati mimi kule nyumbani kwangu ni neema
tupu ya vyakula kedekede. Yaani nimezungukwa
na kila aina ya raha na anasa, na iwapo utakubali kufuatana nami nyumbani, kama
ninavyoamini utakubali, nawe utapata kufaidi sehemu ya mapochopocho yangu.”
Kwa
maneno yale, Panya Pori akashawishika kiurahisi, na akakubali kuandamana
na rafiki yake katika safari ya kurudi mjini. Walipofika, Panya wa Mjini
akamtengea rafikiye mlo wa mkate, shayiri, maharagwe, matini yaliyokaushwa, asali,
zabibu kavu, na, mwishowe, alimletea kipande kinono cha jibini toka kapuni. Panya Pori, akiwa na furaha isiyo kifani kwa kupata chakula kizuri na kingi kama
kile, alishukuru kwa unyenyekevu na kuyalaani maisha yake magumu kule shamba.
Basi wakiwa ndo wanataka kuanza kula, bwana mmoja akafungua mlango, na wote
wawili wakatimka mbio kadri ya uwezo wao na kuingia kwenye kijishimo chembamba
kilichowatosha kwa kujibana. Baadaye wakatoka, na kwa mara nyingine kabla hata
hawajaanza kula, mtu mwingine akafungua mlango na kuingia kuchukua kitu fulani
kabatini, ambapo wale panya wawili, wakiwa na hofu zaidi ya mara ya kwanza,
walikimbia na kwenda kujificha tena.
Mwishowe yule Panya Pori, huku akitweta na akiwa
ameshikwa na njaa kwelikweli, akamwambia rafiki yake:
“Japokuwa umeniandalia
mlo maridhawa, sina budi kuondoka na kukuachia uufaidi mwenyewe. Chakula chako kimezungukwa
na hatari nyingi mno, siwezi kukifurahia hata kidogo. Kwangu mimi ni heri maisha ya kuokoteza nafaka na
kuguguna mizizi porini, ambako ninaishi kwa usalama, bila hofu yoyote.”
Akaenda zake.
***
0 maoni:
Chapisha Maoni