Hadithi za kale zenye mafundisho za Esopo zilizoandikwa zaidi ya miaka 3000 iliyopita. Zimetafsiriwa kwa Kiswahili na Issa S. Kanguni, chini ya shirika lisilo la kiserikali la Tanzania Inventors and Techno-Thinkers Consortium (TITC). Tel; +255757242960

Tafuta katika Blogu Hii

Pages

KISA CHA MZALENDO MWENYE KIPAJI

Ambrose Bierce (1842-1914) Imetafsiriwa na Issa Kanguni (2017).

    Baada ya kufanikiwa kupewa nafasi ya kusikilizwa na mfalme na baraza lake la washauri, bwana mmoja Mzalendo mwenye kipaji cha ubunifu alitoa karatasi mfukoni mwake, akasema: 
    "Kwa ruhusa na mapenzi yako ee Mfalme, ninayo hapa kanuni na michoro ya namna ya kuunda ngao madhubuti za deraya ambazo hakuna risasi wala kombora toka kwenye bunduki yoyote inaweza kupenya. Ngao hizi zikikubaliwa na kuanza kutumiwa na Jeshi letu, basi meli zetu za kivita zitakuwa na ulinzi kamili na hivyo hazitoshindwa na adui yeyote. Hapa, pia, kuna ripoti za baadhi ya Mawaziri wako ewe Mfalme, wakithibitisha thamani na umuhimu wa uvumbuzi huu. Nipo tayari kuuza hakimiliki yangu endapo nitalipwa kiasi cha fedha cha tumtum milioni moja." 

    Baada ya kukagua na kuhakiki makaratasi yale, Mfalme alimwahidi yule bwana kwamba ataagiza Mhazini Mkuu kupitia idara husika amlipe kiasi hicho cha tumtum milioni moja. 

    "Na hii," alisema Mzalendo mwenye kipaji, huku akitoa karatasi nyingine kwenye mfuko mwingine wa suruali yake, "ni kanuni na michoro ya uundaji wa bunduki niliyoivumbua, ambayo ina uwezo wa kupiga risasi ikapenya kwenye ngao hiyo ya deraya. Na hasimu wako ewe Mfalme, ambaye ni Mfalme wa himaya ya Bang, ana shauku kubwa ya kutaka kuinunua, ila utiifu wangu kwa himaya yako ewe Mfalme umenifanya nisite kumuuzia yeye na badala yake nilete kwanza kwako Mkuu. Bei yake ni tumtum milioni moja." 

    Baada ya kuahidiwa muamala mwingine wa malipo, akaingiza mkono kwenye mfuko mwingine wa suruali yake akisema: 
    "Ewe Mfalme, bei ya hiyo bunduki isiyozuilika kwa ngao yoyote ingekuwa kubwa zaidi, laiti isingelikuwa kwamba risasi zake zina uwezekano wa kuzuiwa zisipenye ngao, kwa kutumia njia yangu maalum niliyoivumbua ya kuimarisha deraya ya ngao kwa ku-" 

Mfalme alimkatiza, na akamwita kwa ishara Waziri wake Mkuu. 
    "Mpekue huyu bwana," akamwagiza "kisha nitaarifu mavazi yake yana jumla ya mifuko mingapi." 

    "Mifuko Arobaini na tatu, ee Mfalme," alisema Waziri huku akikamilisha upekuzi wake. 
    Mfalme alighadhabika.

    "Ni vema ukatambua ee Mfalme," yule bwana alisema huku akilia kwa hofu, "kwamba kati ya mifuko hiyo mmoja una tumbaku tu." 

Ndipo Mfalme akaamrisha;
    "Mshikeni huyu bwana kichwa chini miguu juu na mumtikise sana," alisema "halafu mkabidhini hundi ya malipo ya fedha ya kiasi cha tumtum milioni arobaini na mbili, na baada ya hapo anyongwe. Kisha tangazeni sheria mpya ya kwamba ni kosa la jinai mtu yeyote katika himaya yangu kuwa mwerevu na mwenye akili."
***

0 maoni:

Chapisha Maoni

Live Traffic Feed

Blogroll

BTemplates.com

Inaendeshwa na Blogger.

Jumla ya Mara Iliyotazamwa

Popular Posts

Kumbukumbu la Blogu