Hadithi za kale zenye mafundisho za Esopo zilizoandikwa zaidi ya miaka 3000 iliyopita. Zimetafsiriwa kwa Kiswahili na Issa S. Kanguni, chini ya shirika lisilo la kiserikali la Tanzania Inventors and Techno-Thinkers Consortium (TITC). Tel; +255757242960

Tafuta katika Blogu Hii

Pages

Jumatatu, 30 Desemba 2013

KISA CHA SIMBA, MBWA MWITU NA MBWEHA

Simba, kutokana na uzee wake, alilala akiwa hoi mgonjwa kwenye pango lake. 
Wanyama wote wa mwituni walikwenda kumwona na kumsalimu mfalme wao, isipokuwa Mbweha. Kwahiyo Mbwa mwitu, ambaye walikuwa na uhasama wa jadi na Mbweha, aliwaza kuwa huo ulikuwa ni wasaa mzuri sana wa kumkomoa. Akabuni hila ya kutoa mashtaka kwa Mfalme Simba kwamba Mbweha hakuwa na adabu kwake yeye ambaye ni mfalme wao wote na kwamba hakuwa na sababu yoyote ya kutokuja kumjulia hali.

Wakati huohuo Mbweha naye akaingia mle ndani na kuyasikia maneno ya Mbwa mwitu kwa Simba. Simba alimwona na akanguruma kwa ghadhabu dhidi yake. Ndipo Mbweha naye akaona huo ulikuwa ni wasaa wake wa kujitetea na kumgeuzia kibao adui yake, akasema,
ee bwana Mfalme mkuu, hivi ni nani kati ya wote waliokuja kukuona katika hali yako ya ugonjwa wamekuwa wa msaada mkubwa kwako kama mimi, ambaye nimesafiri nchi na nchi, nikaelekea kila upande, nikitafuta na kujifunza toka kwa matabibu dawa ya kukuponya ewe Mfalme wangu?”

Simba akamwamuru amtajie dawa hiyo aliyoigundua mara moja; kabla hajafikiria adhabu ya kumpa kutokana na kuchelewa kwake kuja kumjulia hali Mfalme.

Mbweha akajibu; “Dawa ya kukuponya ee Mfalme ninaijua, na ni ya uhakika kabisa. Itakulazimu ufanye ifuatavyo; Umchune Mbwa mwitu angali yu hai na kisha ujitande ngozi yake ingali ya vuguvugu. Utapona kabisa maradhi yako, na pia utaishi miaka mingi bila kupatwa kamwe na ugonjwa kama huu.”

Simba, kutokana na mateso aliyoyapata na hali mbaya aliyokuwa nayo wakati ule, alijikuta akipata tumaini ghafla kwa dawa ile ya Mbweha. Japo hakuwa na uhakika nayo, alitaka kuijaribu ili aokoe maisha yake.

Mbwa mwitu alikamatwa mara moja na akachunwa ngozi kikatili akiwa hai; ilhali Mbweha alimgeukia, akamwambia huku akitabasamu, “Ulipaswa kumfariji Mfalme wako kwa maneno mazuri ya faraja na kumtia moyo badala ya maneno ya fitina yenye kuchukiza na kukera.”

Hadithi hii inatufundisha nini?
1……………………………………………………………………………………………………………………
2……………………………………………………………………………………………………………………
3……………………………………………………………………………………………………………………
Taja methali, nahau au msemo wa Kiswahili wenye maana inayofanana na maudhui ya hadithi hii;
………………………………………………………………………………………………………………………
………………………………………………………………………………………………………………………

Share:

0 maoni:

Chapisha Maoni

Live Traffic Feed

Blogroll

BTemplates.com

Inaendeshwa na Blogger.

Jumla ya Mara Iliyotazamwa

Popular Posts

Kumbukumbu la Blogu