Maksai, hapo
zamani za kale, waliazimia kufanya hila ya kuwashambulia ghafla na
kuwaangamiza Wachinja ng’ombe wote, kwa kuwa walikuwa wanaendesha
biashara inayoteketeza jamii yao. Azimio hilo lilipitishwa kwa wingi
mkubwa wa kura na maandalizi ya utekelezaji wake yakaanza mara moja.
Siku ya siku
ilipofika walikusanyika ili waweze kutekeleza azma hiyo ya mauaji ya
kushtukiza. Walinoa pembe zao vizuri kujiandaa kwa mapambano. Hamasa
ilikuwa kubwa, na vijana walichagizwa kukaa mstari wa mbele.
Lakini miongoni mwao kulikuwako Maksai mmoja ambaye
alikuwa mzee sana kwa umri (na wingi wa mashamba aliyokwishalima
katika maisha yake) akawaasa kwa kuwaambia: “Ni kweli, Wachinja
ng’ombe hawa wanatuchinja na kutuua, lakini tusisahau kuwa
wanafanya hivyo kwa ujuzi na taaluma ya hali ya juu, na hivyo
hutuepusha na maumivu yasiyo ya lazima. Endapo tutawashambulia na
kuwaangamiza, tutaangukia mikononi mwa wafanyabiashara wasio na ujuzi
wa kuchinja, na tutaanza kuuawa kwa nyundo na mashoka, kwa mateso na
maumivu makali. Itakuwa ni kifo mara mbili zaidi: kwani hakika
nawaambieni, ingawa tutawaangamiza Wachinja Ng’ombe wote, bado
binadamu wataendelea kuhitaji nyama ya ng’ombe daima.”
0 maoni:
Chapisha Maoni