Hapo zamani
kulikuwepo mtu mmoja tajiri aliyeheshimika sana na watu wa jamii
yake. Bwana huyo alifungua majumba ya maonyesho ya sanaa na watu wote
waliruhusiwa kuingia bure. Wake kwa waume, watoto na wakubwa. Ikawa
baada ya kazi nyingi za kutwa za kujitafutia riziki, Wananchi
wakapata burudani na kufurahi pamoja.
Ila kwa kuwa
maonyesho yalifanyika mara kwa mara, na wasanii walikuwa ni wale
wale, na burudani ni zilezile zikijirudiarudia, siku zilipopita mambo
yalianza kwenda doro kwa idadi ya wahudhuriaji kupungua na msisimko
nao kushuka.
Yule tajiri
alifikiri namna ya kufanya ili kuwarudisha watu katika uchangamfu
kama awali.
Siku moja
alitoa tangazo kwa umma akiahidi kutoa zawadi nono sana kwa mtu
yeyote atakayeweza kufanya uvumbuzi wa aina mpya kabisa ya burudani
jukwaani.
Watu kemkem
wenye uzoefu katika tasnia ya kuburudisha umma kwa nyimbo, maigizo,
vichekesho nk; walijitokeza kuishindania zawadi ile.
Miongoni mwao
alikuwapo Mchekeshaji ambaye alikuwa maarufu sana kutokana na
vichekesho vyake mahiri.
Alijitokeza
na kusema kuwa yeye ana aina mpya kabisa ya burudani ambayo
haijawahi kuonyeshwa jukwaani kabla. Na wala hakuna mtu yeyote
atakayeweza kushindana naye. Alijigamba, na walio wengi walimwamini.
Habari ile
ilisambaa kama upepo na kuleta hamasa kubwa, ikawa gumzo kila pahali.
Na siku ya shindano ilipofika ukumbi ulijaa ukatapika. Waliochelewa
kufika walilazimika kusikiliza wakiwa nje.
Kila kitu
kiliandaliwa vizuri na muda ulipofika mambo yakajiri kama
ilivyopangwa.
Baada ya
wengine kutoa burudani zao, kila mtu akishangiliwa na kutuzwa kwa
kadiri yake, ikafika zamu ya yule aliyekuwa akisubiriwa kwa hamu.
Mchekeshaji
alitokea jukwaani peke yake, bila kifaa cha aina yoyote wala
washirika. Shauku kubwa ya matarajio chanya vilipelekea ukumbi
kugubikwa na kimya kikuu. Watu wakisubiri kwa hamu kushuhudia
kichekesho kipya walichoahidiwa na msanii yule nguli. Akiwa
amevalia joho lake refu la rangi ya hudhurungi, ghafla alijipinda na
kuinamisha kichwa chake kuelekea tumboni, kisha akatoa sauti kali ya
kuiga mlio wa kitoto cha Nguruwe. Mlio huo aliouiga kwa sauti yake
ulikuwa wa kupendeza kiasi kwamba hadhira ile ikamshuku kuwa huenda
alikuwa ameficha kitoto cha Nguruwe kwenye vazi lake pana. Wakadai
akaguliwe ili kuhakikisha, kabla hawajampa sifa na kumtawaza kuwa ni
mshindi halali wa zawadi inayoshindaniwa.
Baada ya
kufanya hivyo na kukutwa hana kitu chochote alichoficha, ukumbi
ulilipuka kwa mayowe ya furaha na kushangilia usanii ule mpya.
Mwanakijiji
mmoja miongoni mwa hadhira alipoyashuhudia yale yote, alipata wazo na
kusema, “Nisaidieni enyi wakuu, mimi pia naweza, najua hawezi
kunishinda katika kuiga sauti kama hii.” Na hapo hapo alitangaza
kuwa ataigiza sauti kama vile siku inayofuata, na itakuwa kwa ubora
na uhalisia zaidi. Na akawaomba wananchi watulie kwani mshindi wa
kweli wa zawadi ile atatambulika baada ya yeye pia kupewa nafasi ya
kusikilizwa.
Kesho yake
umati mkubwa zaidi ulifurika kwenye jumba la maonyesho, wakiwa na
mapenzi na ushabiki kwa Mchekeshaji, na wengi walikuja kwa lengo la
kutaka kumdhihaki na kumsuta Mwanakijiji, na sio kushuhudia uwezo
wake wa kuiga sauti vizuri kuzidi ile ya msanii aliyepita.
Wasanii wote
walitokea jukwaani. Mchekeshaji alikuwa wa kwanza, alijiinamia
tumboni na kuiga sauti ya kitoto cha nguruwe, kama siku iliyopita, na
hadhira ilimshangilia sana kwa mbinja na vifijo.
Ndipo
Mwanakijiji akapewa nafasi, akainama na kujifanya kama ameficha
kitoto cha nguruwe kwenye vazi lake (ambapo ni kweli alikificha, ila
hakuna aliyemshuku) alishika na kuyanyonga masikio, na mlio mkali wa
kitoto cha nguruwe ulisikika.
Watazamaji,
hata hivyo, walipaza sauti kwa pamoja wakisema kuwa yule Mchekeshaji
aliyepita ndiye mshindi kwani aliiga mlio wa kitoto cha nguruwe kwa
ufasaha zaidi. Wakataka Mwanakijiji aburuzwe nje ya jumba lile. Ndipo
yule mshamba akakitoa kitoto halisi cha nguruwe kwenye mavazi yake,
na kuionyesha hadhira ushahidi chanya kuhusu upotofu wa hukumu
waliyotoa.
“Tazameni,” alisema, “hii inadhihirisha wazi ninyi
ni aina gani ya mahakimu!”
Hadithi hii
inatufundisha nini?
1……………………………………………………………………………………………………………………
2……………………………………………………………………………………………………………………
3……………………………………………………………………………………………………………………
Taja methali, nahau au
msemo wa Kiswahili wenye maana inayofanana na maudhui ya hadithi
hii;
………………………………………………………………………………………………………………………
………………………………………………………………………………………………………………………
0 maoni:
Chapisha Maoni