Hadithi za kale zenye mafundisho za Esopo zilizoandikwa zaidi ya miaka 3000 iliyopita. Zimetafsiriwa kwa Kiswahili na Issa S. Kanguni, chini ya shirika lisilo la kiserikali la Tanzania Inventors and Techno-Thinkers Consortium (TITC). Tel; +255757242960

Tafuta katika Blogu Hii

Pages

Jumapili, 18 Mei 2014

KISA CHA TAI, PAKA NA NGURUWE PORI

Kulitokea Tai mmoja ambaye alijenga kiota chake juu ya mti mkubwa; Paka naye, baada ya kuona kuna shimo linalomfaa, alihamia na kuanza kuishi katikati ya shina la mti ule ule; na Nguruwe pia, akiwa na vitoto vyake, akaweka makazi kwenye shimo lililopo wazi chini ya mti ule. 

Basi ikawa Paka, kwa tabia yake mbaya, akaanza kutengeneza hila ili kuvuruga kusanyiko lile la kudra la familia tatu tofauti katika mti mmoja. Ili kutekeleza njama yake, alianza kwa kupanda juu kwenye kiota cha Tai, akamwambia, 
"Ndugu yangu, angamizo linakaribia kushuka juu yako, na mimi pia, kwa bahati mbaya. Jirani yetu Nguruwe-pori, ambaye unamwona kila siku akichimbua chimbua ardhi kwa mdomo wake, anataka kuung'oa mti huu, ili utakapoanguka akamate familia yako na yangu kwa ajili ya chakula kwa watoto wake." 

Baada ya kufanikiwa kumwogofya Tai kiasi kile, Paka alishuka chini kabisa na kwenda kwenye shimo la Nguruwe-pori, akamwambia, "Ndugu yangu, maisha ya watoto wako yapo hatarini; kwani punde tu utakapothubutu kutoka kwenda kutafuta chakula, Tai amejiandaa kushambulia mmoja wa watoto wako, kwa ajili ya chakula cha familia yake." 
Alipofanikiwa kumjaza hofu Nguruwe-pori, Paka akaenda zake kwake na kujifanya kana kwamba naye anajificha kwa woga kwenye shimo lake. Ilipofika nyakati za usiku kila siku alinyata na kutoka kinyemela kwenda kutafuta chakula kwa ajili yake na wanawe, huku akijifanya kuogopa na kuwalinda wanawe mchana kutwa.

Wakati huo, Tai,  akiwa ana hofu kuu dhidi ya Nguruwe-pori, alikaa kwenye kiota chake kutwa kucha, ilhali Nguruwe pori naye, akiwa na hofu kuu dhidi ya Tai, hakuthubutu kutoka kwenye shimo lake. 
Kwa hali hiyo, wote pamoja na familia zao, waliangamia kwa njaa, na kumwacha Paka na wanawe wakijivinjari kwa nafasi.
***
Share:

0 maoni:

Chapisha Maoni

Live Traffic Feed

Blogroll

BTemplates.com

Inaendeshwa na Blogger.

Jumla ya Mara Iliyotazamwa

Popular Posts

Kumbukumbu la Blogu