Bwana mmoja bahili aliuza vitu vyake vyote alivyonavyo na kununua sarafu za dhahabu, ambazo alichimba shimo na kuzifukia chini kando ya ukuta wa zamani na kuwa anakwenda kuziangalia kila siku. Mmoja wa wafanyakazi wake aligundua safari zake za mara kwa mara kwenda eneo lile na akaanza kumchunguza zaidi.
Muda mfupi tu baadaye aling'amua siri ya ile hazina iliyofichwa, na alipochimbua na kukuta rundo la dhahabu, akaziiba. Yule bwana bahili, alipofika siku iliyofuata, alikuta shimo tupu na akaanza kulia na kuvuta nywele zake hata kuzinyofoa kwa hasira na majonzi. Jirani yake, baada ya kumwona akiwa katika hali ile ya huzuni kupita kiasi, na alipogundua sababu ya huzuni ile, alimwambia
"Ndugu, hakuna haja ya kuhuzunika kiasi hicho; bali nenda na uchukue jiwe, liweke humo shimoni na ufunike, kishakila siku kuangalia na jifanye kana kwamba dhahabu zako bado zimo humo. Itakufaa kwa hali ile ile; kwani hata kabla ya kuibiwa haukuwa nayo dhahabu, kwa kuwa uliifukia tu na hukuitumia kwa namna yoyote ile."
***
0 maoni:
Chapisha Maoni