Hapo zamaini za kale, kulitokea Mbweha
mmoja mjanja. Siku moja kwenye pitapita zake kwa bahati mbaya alinaswa mtegoni, na katika kuhangaika
alifanikiwa kujinasua, ila alikatika mkia ukabakia kipisi kifupi tu.
Siku za
mwanzo mwanzo aliona aibu kujionyesha ulemavu wake wa kutokuwa na mkia kwa mbweha wenzake. Baadaye akaamua
kujibaraguza na kufanya kana kwamba kukosa mkia si kitu, akawaalika Mbweha wote
kwenye mkutano mkuu, ili wajadili pendekezo alilo nalo moyoni.
Walipokusanyika,
Mbweha alitangaza pendekezo lake, kwamba eti mbweha wote ni vyema wakakata
mikia yao na kubaki na vipisi kama yeye. Akasema kwamba mkia ni mzigo wanapokuwa
wanafukuzwa na maadui zao, mbwa; na pia unasumbua wanapohitaji kuketi kitako
wazungumze mambo kirafiki na wenzi wao. Akapaza sauti na kudai kuwa haoni faida yoyote ya wao kuendelea kubeba zigo la mkia usio na tija yoyote.
“Hiyo ni sawa kabisa,”
akajibu mbweha mmoja mzee; “ila sidhani kama ungelitoa pendekezo la kukata
mikia ambayo ni kifaa chetu muhimu, laiti kama wewe mwenyewe usingalipatwa janga
la kupoteza mkia wako.”
***
0 maoni:
Chapisha Maoni