Hadithi za kale zenye mafundisho za Esopo zilizoandikwa zaidi ya miaka 3000 iliyopita. Zimetafsiriwa kwa Kiswahili na Issa S. Kanguni, chini ya shirika lisilo la kiserikali la Tanzania Inventors and Techno-Thinkers Consortium (TITC). Tel; +255757242960

Tafuta katika Blogu Hii

Pages

Alhamisi, 30 Januari 2014

HADITHI YA BIBI KIZEE NA CHUPA YA MVINYO

Bibi kizee aliokota chupa tupu ya mvinyo ambayo alitambua kuwa siku nyingi zilizopita ilijaa mvinyo. Ila alishangaa kuona kuwa hadi wakati huo ilikuwa ikitoa harufu mzuri ya kinywaji hicho.

Kwa uchu, aliisogeza chupa hiyo puani na kuvuta harufu yake, akaitazama, kisha akarudia kuinusa mara kadhaa na kusema kwa husuda,
Oo… kinywaji murua kabisa! Yamkini huu ulikuwa Mvinyo maridadi kwelikweli, kwa maana umeacha kwenye chupa hii harufu nzuri sana ya manukato!”

Hadithi hii inatufundisha nini?
1……………………………………………………………………………………………………………………
2……………………………………………………………………………………………………………………
3……………………………………………………………………………………………………………………
Taja methali, nahau au msemo wa Kiswahili wenye maana inayofanana na maudhui ya hadithi hii;
………………………………………………………………………………………………………………………
………………………………………………………………………………………………………………………

Share:

KISA CHA NG'OMBE NA CHURA

Ng’ombe Maksai alikwenda kunywa maji katika dimbwi ambalo lilikuwa na watoto wa chura. Watoto hao walizaliwa hapo na kwao hiyo ilikuwa ni maskani yao halali. Ila kwa wakati ule mama yao alikuwa ametoka, kaenda kuitembelea familia ya rafiki yake iliyokuwa na makazi kwenye dimbwi jingine upande wa pili wa kichaka.

Kwa bahati mbaya, Maksai alimkanyaga mtoto mmoja wa Chura na kumjeruhi vibaya, akafa. Punde mama yao akarejea toka matembezini na kubaini kuwa mmoja wa watoto wake hayupo dimbwini. Akawauliza wale nduguze kulikoni.

Mwenzetu amekufa, mama mpenzi;” alijibu mmoja wao kwa majonzi.
Kumetokea nini tena mbona niliwaacha wote wazima?” mama Chura alihoji.
Muda si mrefu uliopita mnyama mkubwa sana alikuja dimbwini akamkanyaga kwa kwato zake kubwa na kumuua.” walimjibu.

Chura alihamaki mno, akaanza kuvuta pumzi na kujitunisha kwa hasira, akahoji, “iwapo baradhuli huyo alikuwa mkubwa kiasi hicho kwa umbo,”
Ee mama yetu mpendwa, acha kujijaza upepo na kujitunisha” mtoto wake mmoja alimkatisha, “na wala usighadhibike kiasi hicho; kwani hakika nakuambia, utaanza kupasuka mwili kabla hujafanikiwa kuiga ukubwa wa dhalimu yule.”

Hadithi hii inatufundisha nini?
1……………………………………………………………………………………………………………………
2……………………………………………………………………………………………………………………
3……………………………………………………………………………………………………………………
Taja methali, nahau au msemo wa Kiswahili wenye maana inayofanana na maudhui ya hadithi hii;
………………………………………………………………………………………………………………………
………………………………………………………………………………………………………………………

Share:

Alhamisi, 2 Januari 2014

HADITHI YA MBWEHA NA CHUI

Siku moja mbweha na chui walizozana kuhusu nani kati yao alikuwa mzuri kuliko mwenzake. Chui alijinadi kwa kumwonyesha mbweha moja baada ya jingine madoa yaliyoipamba na kuipendezesha ngozi yake. Na kweli ukimwangalia Chui na madoa yake alionekana mzuri anayevutia.

Lakini mbweha naye alimkatiza kwa kusema, “hivi ni nani mzuri kati yako wewe, na mimi ambaye sijapambwa ngozi bali nimepambwa roho?”

Chui akaduwaa.

Hadithi hii inatufundisha nini?
1……………………………………………………………………………………………………………………
2……………………………………………………………………………………………………………………
3……………………………………………………………………………………………………………………
Taja methali, nahau au msemo wa Kiswahili wenye maana inayofanana na maudhui ya hadithi hii;
………………………………………………………………………………………………………………………
………………………………………………………………………………………………………………………

Share:

KISA CHA MWANADAMU NA SIMBA

Mwanadamu na Simba walikuwa wakisafiri pamoja kuelekea upande mwingine wa nchi. Wakiwa safarini walianza kutambiana, kila mmoja akijigamba kuwa ni mkuu na mwenye ushujaa na umahiri.

Wakati wakiendelea kubishana, walipita mahali ambapo kulikuwa na sanamu kubwa ya mawe ikimwonyesha “Simba akinyongwa na binadamu.” Msafiri yule alimwonyesha Simba sanamu ile na kusema kwa majivuno: “Unaona!... jinsi ambavyo binadamu tuna nguvu, na jinsi tunavyoweza kumshinda hata mfalme wa wanyama wote.”

Simba akamjibu: “Sikiliza rafiki yangu nikupashe, Sanamu hii tuionayo mbele yetu imechongwa na mmoja kati ya Binadamu. Laiti kama nasi Simba tungelikuwa na ujuzi wa kuchonga sanamu, ungeona sanamu ya Binadamu akiwa amefinywa chini ya kiganja cha Simba.”

Hadithi hii inatufundisha nini?
1……………………………………………………………………………………………………………………
2……………………………………………………………………………………………………………………
3……………………………………………………………………………………………………………………
Taja methali, nahau au msemo wa Kiswahili wenye maana inayofanana na maudhui ya hadithi hii;
………………………………………………………………………………………………………………………
………………………………………………………………………………………………………………………
Share:

KISA CHA MCHEKESHAJI NA MWANAKIJIJI

Hapo zamani kulikuwepo mtu mmoja tajiri aliyeheshimika sana na watu wa jamii yake. Bwana huyo alifungua majumba ya maonyesho ya sanaa na watu wote waliruhusiwa kuingia bure. Wake kwa waume, watoto na wakubwa. Ikawa baada ya kazi nyingi za kutwa za kujitafutia riziki, Wananchi wakapata burudani na kufurahi pamoja.

Ila kwa kuwa maonyesho yalifanyika mara kwa mara, na wasanii walikuwa ni wale wale, na burudani ni zilezile zikijirudiarudia, siku zilipopita mambo yalianza kwenda doro kwa idadi ya wahudhuriaji kupungua na msisimko nao kushuka.

Yule tajiri alifikiri namna ya kufanya ili kuwarudisha watu katika uchangamfu kama awali.
Siku moja alitoa tangazo kwa umma akiahidi kutoa zawadi nono sana kwa mtu yeyote atakayeweza kufanya uvumbuzi wa aina mpya kabisa ya burudani jukwaani.
Watu kemkem wenye uzoefu katika tasnia ya kuburudisha umma kwa nyimbo, maigizo, vichekesho nk; walijitokeza kuishindania zawadi ile. 

Miongoni mwao alikuwapo Mchekeshaji ambaye alikuwa maarufu sana kutokana na vichekesho vyake mahiri.
Alijitokeza na kusema kuwa yeye ana aina mpya kabisa ya burudani ambayo haijawahi kuonyeshwa jukwaani kabla. Na wala hakuna mtu yeyote atakayeweza kushindana naye. Alijigamba, na walio wengi walimwamini.
Habari ile ilisambaa kama upepo na kuleta hamasa kubwa, ikawa gumzo kila pahali. Na siku ya shindano ilipofika ukumbi ulijaa ukatapika. Waliochelewa kufika walilazimika kusikiliza wakiwa nje.

Kila kitu kiliandaliwa vizuri na muda ulipofika mambo yakajiri kama ilivyopangwa.
Baada ya wengine kutoa burudani zao, kila mtu akishangiliwa na kutuzwa kwa kadiri yake, ikafika zamu ya yule aliyekuwa akisubiriwa kwa hamu.

Mchekeshaji alitokea jukwaani peke yake, bila kifaa cha aina yoyote wala washirika. Shauku kubwa ya matarajio chanya vilipelekea ukumbi kugubikwa na kimya kikuu. Watu wakisubiri kwa hamu kushuhudia kichekesho kipya walichoahidiwa na msanii yule nguli. Akiwa amevalia joho lake refu la rangi ya hudhurungi, ghafla alijipinda na kuinamisha kichwa chake kuelekea tumboni, kisha akatoa sauti kali ya kuiga mlio wa kitoto cha Nguruwe. Mlio huo aliouiga kwa sauti yake ulikuwa wa kupendeza kiasi kwamba hadhira ile ikamshuku kuwa huenda alikuwa ameficha kitoto cha Nguruwe kwenye vazi lake pana. Wakadai akaguliwe ili kuhakikisha, kabla hawajampa sifa na kumtawaza kuwa ni mshindi halali wa zawadi inayoshindaniwa.

Baada ya kufanya hivyo na kukutwa hana kitu chochote alichoficha, ukumbi ulilipuka kwa mayowe ya furaha na kushangilia usanii ule mpya.
Mwanakijiji mmoja miongoni mwa hadhira alipoyashuhudia yale yote, alipata wazo na kusema, “Nisaidieni enyi wakuu, mimi pia naweza, najua hawezi kunishinda katika kuiga sauti kama hii.” Na hapo hapo alitangaza kuwa ataigiza sauti kama vile siku inayofuata, na itakuwa kwa ubora na uhalisia zaidi. Na akawaomba wananchi watulie kwani mshindi wa kweli wa zawadi ile atatambulika baada ya yeye pia kupewa nafasi ya kusikilizwa.

Kesho yake umati mkubwa zaidi ulifurika kwenye jumba la maonyesho, wakiwa na mapenzi na ushabiki kwa Mchekeshaji, na wengi walikuja kwa lengo la kutaka kumdhihaki na kumsuta Mwanakijiji, na sio kushuhudia uwezo wake wa kuiga sauti vizuri kuzidi ile ya msanii aliyepita.
Wasanii wote walitokea jukwaani. Mchekeshaji alikuwa wa kwanza, alijiinamia tumboni na kuiga sauti ya kitoto cha nguruwe, kama siku iliyopita, na hadhira ilimshangilia sana kwa mbinja na vifijo.
Ndipo Mwanakijiji akapewa nafasi, akainama na kujifanya kama ameficha kitoto cha nguruwe kwenye vazi lake (ambapo ni kweli alikificha, ila hakuna aliyemshuku) alishika na kuyanyonga masikio, na mlio mkali wa kitoto cha nguruwe ulisikika.

Watazamaji, hata hivyo, walipaza sauti kwa pamoja wakisema kuwa yule Mchekeshaji aliyepita ndiye mshindi kwani aliiga mlio wa kitoto cha nguruwe kwa ufasaha zaidi. Wakataka Mwanakijiji aburuzwe nje ya jumba lile. Ndipo yule mshamba akakitoa kitoto halisi cha nguruwe kwenye mavazi yake, na kuionyesha hadhira ushahidi chanya kuhusu upotofu wa hukumu waliyotoa.

Tazameni,” alisema, “hii inadhihirisha wazi ninyi ni aina gani ya mahakimu!”

Hadithi hii inatufundisha nini?
1……………………………………………………………………………………………………………………
2……………………………………………………………………………………………………………………
3……………………………………………………………………………………………………………………
Taja methali, nahau au msemo wa Kiswahili wenye maana inayofanana na maudhui ya hadithi hii;
………………………………………………………………………………………………………………………
………………………………………………………………………………………………………………………

Share:

HADITHI YA TAI NA MBWEHA

Tai na Mbweha walikuwa marafiki wapenzi na hivyo walikubaliana kutoishi mbalimbali. Wakautafuta mti mmoja mzuri. Tai akajenga kiota chake kwenye matawi ya mti huo mkubwa, wakati Mbweha aliweka makazi yake kwenye shimo chini ya mti huo huo. Miezi michache baadaye Mbweha alizaa vitoto vinne.

Muda si mrefu baada ya makubaliano yao ya kuishi jirani kwa urafiki, Tai, kutokana na mahitaji yake ya chakula cha kuwalisha makinda wake, alishuka chini ya mti wakati rafiki yake Mbweha yupo matembezini, akakamata kitoto kimoja cha Mbweha, akakiua na kukila yeye na wanawe.

Mbweha aliporudi, aligundua kilichotokea, akahuzunika sana. Huzuni yake kuu haikuwa tu kwa kifo cha mtoto wake, bali pia ni jinsi ambavyo hakuwa na uwezo wa kulipiza kisasi kwa ukatili aliofanyiwa na rafiki yake, kwani asingeweza kupanda juu kwenye kiota cha Tai.

Hata hivyo muda si mrefu baadaye malipo ya udhalimu yalimfika Tai.
Akirukaruka kwenye mawindo sehemu fulani , ambako wanakijiji walikuwa wakitoa dhabihu ya mbuzi, ghafla akashuka na kudokoa pande la nyama, na kulichukua, pamoja na kizinga cha moto kilichoambatana nayo, bila kujua hadi kwenye kiota chake. Upepo mkali uliopovuma uliwasha moto kwenye kiota, hivyo wale makinda wake, kwa kuwa hawakuwa na mbawa bado, walishindwa kujiokoa wakaungua na kubanikwa kwenye kiota chao wakafa na kudondoka chini ya mti. 

Hapo chini, huku mama yao Tai akishuhudia, Mbweha akawala wote kwa kisasi.
Naye Tai alihuzunika sana.

Hadithi hii inatufundisha nini?
1……………………………………………………………………………………………………………………
2……………………………………………………………………………………………………………………
3……………………………………………………………………………………………………………………
Taja methali, nahau au msemo wa Kiswahili wenye maana inayofanana na maudhui ya hadithi hii;
………………………………………………………………………………………………………………………
………………………………………………………………………………………………………………………

Share:

KISA CHA MUUAJI

Mtu mmoja alimjeruhi mwenzie na kumuua. Ndugu na jamaa wa marehemu walianza kumkimbiza wakiwa na silaha kwa minajili la kumuua kwa kisasi.

Yule muuaji alikimbia kwa bidii kuu ili aokoe roho yake na hatimaye akafika kwenye kingo ya mto Nile. Ng’ambo ya mto alimwona Simba na kwa woga wake wa kuhofia kuuawa akaamua kukwea juu ya mti.

 Kule mtini pia aliona Joka kubwa kwenye matawi ya juu kwenye kilele, akaogopa sana kuuawa kwa sumu. Akaamua kujitupa mtoni ambako nako kulikuwa na Mamba. 

Alishikwa akauawa na kuliwa papo hapo.

Hivyo ardhi, anga na maji vyote kwa pamoja vilikataa kumficha Mwuaji yule.

Hadithi hii inatufundisha nini?
1……………………………………………………………………………………………………………………
2……………………………………………………………………………………………………………………
3……………………………………………………………………………………………………………………
Taja methali, nahau au msemo wa Kiswahili wenye maana inayofanana na maudhui ya hadithi hii;
………………………………………………………………………………………………………………………
………………………………………………………………………………………………………………………
Share:

HADITHI YA SIMBA, MBWEHA NA WANYAMA WENGINE

Siku moja Simba alitangaza kuwa yu mgonjwa mahtuti na kwamba alikaribia kufa. Hivyo alitoa tamko la kuwaalika Wanyama wote waende nyumbani kwake kumwona na kusikia wosia wake wa mwisho na ushuhuda wa mambo kadha wa kadha, na pia wapate busara za mfalme.

Hivyo Mbuzi alienda kwenye pango alililoishi Mfalme Simba ili kumjulia hali. Alisimama kwenye sehemu ya kuingilia pangoni na kusikiliza kwa muda mrefu. Kisha kondoo alikuja na akaingia pangoni moja kwa moja, na kabla hajatoka Mwanafarasi naye alikuja kupokea wosia wa mwisho wa Mfalme, akaingia pangoni.

Baada ya muda mfupi Simba alijitokeza nje akionekana kupata nafuu ya haraka, akaja kwenye lango lake la kuingilia pangoni ili apunge upepo wa nje. Alipopiga macho kushoto na kulia alimwona Mbweha, akiwa amejiinamia anasubiri nje ya pango kwa muda mrefu.

Kwa nini ewe Mbweha hujaja ndani ya pango kutoa heshima zako za mwisho kwangu? Na badala yake unakaa tu hapa nje kwa kejeli?” Simba alimuuliza.

Nisamehe Bwana mkubwa,” Mbweha alijitetea, “ila katika kuja kwangu hapa nimegundua alama za nyayo za wanyama wengi ambao wamekwisha kukutembelea pangoni mwako; na nikichunguza kwa makini zaidi naona alama nyingi za kwato zikiingia ndani, na sioni zitokazo nje. Hadi hapo nitakapowaona wanyama waliokwishaingia pangoni mwako wakitoka nje, sitoingia, naona ni heri nibaki hukuhuku nje kwenye uwazi na hewa safi.”

Hadithi hii inatufundisha nini?
1……………………………………………………………………………………………………………………
2……………………………………………………………………………………………………………………
3……………………………………………………………………………………………………………………
Taja methali, nahau au msemo wa Kiswahili wenye maana inayofanana na maudhui ya hadithi hii;
………………………………………………………………………………………………………………………
………………………………………………………………………………………………………………………

Share:

Live Traffic Feed

Blogroll

BTemplates.com

Inaendeshwa na Blogger.

Jumla ya Mara Iliyotazamwa

Popular Posts

Kumbukumbu la Blogu