Hadithi za kale zenye mafundisho za Esopo zilizoandikwa zaidi ya miaka 3000 iliyopita. Zimetafsiriwa kwa Kiswahili na Issa S. Kanguni, chini ya shirika lisilo la kiserikali la Tanzania Inventors and Techno-Thinkers Consortium (TITC). Tel; +255757242960

Tafuta katika Blogu Hii

Pages

Jumanne, 31 Desemba 2013

HADITHI YA MTOTO NA MBWA MWITU

Mtoto mmoja, akiwa anarudi peke yake kutoka machungani wakati wa jioni, alipita katikati ya kichaka ambako alikutana na Mbwa mwitu. Kumbe yule Mbwa mwitu alikuwa na njaa na alijua kuwa mtoto kama yule angetosha kabisa kwa chakula cha jioni kwake na kwa familia yake ya watoto wanne kule pangoni. Alianza kumnyemelea akimmezea mate kwa uchu.

Yule mtoto aliogopa sana, mwili mzima ulitetema, ingawa alijitia ujasiri na hakutaka kufa kikondoo. Alifahamu ya kuwa hawezi kupambana naye kwa mabavu akamshinda, wala asingeliweza kushindana naye kwa mbio akamzidi.

Hivyo alipoona kwamba hakuwa na namna ya kujiepusha na hatari ile, alimgeukia Mbwa mwitu na kumwambia kwa unyenyekevu: “Najua, ee rafiki yangu Mbwa mwitu, ya kwamba u na njaa na mimi ni windo lako, na kwa kuwa sina uwezo wowote wa kujiokoa dhidi yako, basi kabla ya kuniua nakuomba unisaidie kitu kimoja tu. Nacho ni uniimbie wimbo mmoja niupendao ili nicheze kwa mara ya mwisho, kisha nikimaliza uniue na kunila.”

Mbwa mwitu aliangua kicheko kusikia ombi la mtoto ambaye kwake alikuwa tayari ni marehemu mtarajiwa. Baadaye alikubali, akachukua filimbi na kuanza kumpigia wimbo.
Wakati mtoto anacheza huku akiwa amejawa na hofu, Mbwa wa nyumbani kwake walisikia sauti ile, wakakimbilia pale kabla ya ule wimbo kwisha na kuanza kumtimua yule Mbwa mwitu.

Mbwa mwitu alimgeukia mtoto akasema, “Hii ni halali yangu; kwani mimi ambaye wasifu wangu ni muuaji na mla nyama, sikupaswa kugeuka mpiga filimbi ili kukidhi matakwa yako wewe.”

Hadithi hii inatufundisha nini?
1……………………………………………………………………………………………………………………
2……………………………………………………………………………………………………………………
3……………………………………………………………………………………………………………………
Taja methali, nahau au msemo wa Kiswahili wenye maana inayofanana na maudhui ya hadithi hii;
………………………………………………………………………………………………………………………
………………………………………………………………………………………………………………………
Share:

Jumatatu, 30 Desemba 2013

KISA CHA SIMBA NA PANYA

Siku moja mfalme Simba akiwa amejipumzisha kivulini, alipitiwa na usingizi. Panya mtukutu alimsogelea na kuanza kuchezacheza juu yake; hali ambayo ilimfanya aamke mara moja. Alipoamka, Simba alimkamata Panya kwa kumkandamiza na guu lake kubwa, tayari kwa kumla.

Naomba unisamehe, ee Mfalme,” Panya alilia na kuomba: “nisamehe kwa sasa na sitosahau kamwe: huwezi kujua pengine ipo siku mimi pia ninaweza kulipa wema wako kwa kukusaidia!.”

Simba aliguswa sana na maneno ya Panya kwamba eti huenda ipo siku akamsaidia yeye Simba, mnyama mkubwa ambaye ni mfalme wa wanyama wote. Aliinua mguu wake na kumwacha aende zake.

Siku moja Simba alinaswa kwenye mtego wa Binadamu, na wawindaji walipomkuta walipanga kumpeleka kwa Mfalme wao kama zawadi akiwa hai vilevile. Walimfunga kwenye mti kwa kamba kisha wakaondoka kwenda kutafuta usafiri wa kumbebea.

Punde ikatokea yule Panya alipita maeneo yale, na alipomwona Simba yupo katika hali ile ya taharuki, majonzi na hofu ya kuuawa, alienda pale mtini na kuzikatakata kwa meno yake makali kamba zile zilizomfunga Mfalme wa wanyama wote.
Si nilikwambia,? unaona sasa…” alisema Panya.

Hadithi hii inatufundisha nini?
1……………………………………………………………………………………………………………………
2……………………………………………………………………………………………………………………
3……………………………………………………………………………………………………………………
Taja methali, nahau au msemo wa Kiswahili wenye maana inayofanana na maudhui ya hadithi hii;
………………………………………………………………………………………………………………………
………………………………………………………………………………………………………………………
Share:

HADITHI YA SEREMALA NA SANAMU YA MEKYURI

Kulikuwa na mtu mmoja fukara sana, kazi yake ni fundi Seremala. Ndani ya nyumba yake pamoja na vitu vingine, aliweka sanamu ya Mekyuri ambaye aliaminika kuwa ni mjumbe wa Mungu. 

Kila siku fukara huyo aliitolea sanamu ile sadaka, na kuiomba imbariki na kumfanya kuwa tajiri. Lakini fundi alizidi tu kuwa fukara siku hadi siku, zaidi na zaidi.
Mwishowe alighadhibika, akaamua kuishusha sanamu ile toka kwenye kiweko chake na kuibamiza ukutani kwa jazba.

Baada ya kichwa cha Sanamu hilo kung’oka, zikamiminika dhahabu chungu nzima, ambazo fundi Seremala alizizoa na kusema, “Ewaa, nadhani sanaa yako kwa ujumla ni ya mkanganyiko na isiyoeleweka; kwani nilipokupa heshima na kukunyenyekea sikupata mali kutoka kwako: ila sasa nimekutenda vibaya umenijazia dhahabu na utajiri tele.”

Hadithi hii inatufundisha nini?
1……………………………………………………………………………………………………………………
2……………………………………………………………………………………………………………………
3……………………………………………………………………………………………………………………
Taja methali, nahau au msemo wa Kiswahili wenye maana inayofanana na maudhui ya hadithi hii;
………………………………………………………………………………………………………………………
………………………………………………………………………………………………………………………

Share:

HADITHI YA MBWEHA NA PAKA

Mbweha alikuwa akijigamba mbele ya Paka kuwa yeye ana mbinu nyingi sana za kuwakwepa maadui zake.
Nina fuko zima la mbinu na ujanja,” alisema, “ambalo lina mamia ya njia za kujiepusha na maadui zangu wakati wa hatari.”

Mimi ninayo mbinu moja tu,” alisema Paka; “lakini ninaiamini, na inanifaa hiyo hiyo.”

Wakiongea maneno hayo, punde wakasikia sauti za Mbwa wawindaji zikielekea upande wao, na Paka alichupa akauparamia mti haraka na kujificha juu kwenye matawi. “Hii ndiyo mbinu yangu,” alisema Paka. “Je mwenzangu wafanyaje?”

Mbweha akafikiri kwanza kutumia njia hii, mara njia ile, na kabla hajafanya maamuzi, Mbwa walimkaribia na kumkaribia, na mwishowe Mbweha akiwa katika mkanganyiko huo, alikamatwa na kuuawa na Wawindaji.

Paka ambaye alikuwa akishuhudia kinachotokea, alisema;
Heri njia moja salama kuliko njia mia ambazo huwezi kuzitumia.”

Hadithi hii inatufundisha nini?
1……………………………………………………………………………………………………………………
2……………………………………………………………………………………………………………………
3……………………………………………………………………………………………………………………
Taja methali, nahau au msemo wa Kiswahili wenye maana inayofanana na maudhui ya hadithi hii;
………………………………………………………………………………………………………………………
………………………………………………………………………………………………………………………
Share:

KISA CHA SUNGURA NA SIMBA

Hapo zamani za kale kulikuwako mkutano mkuu wa wanyama kila baada ya miaka mitatu, ambapo wanyama wote walipata fursa ya kutoa michango ya mawazo ili kuboresha kanuni na namna ya maisha yao kama jamii moja.

Siku moja, wakiwa katika mkutano kama huo, Sungura walitoa mawaidha kwa hisia kali sana, rai yao ikiwa ni kutaka wanyama wote wawe na haki sawa.

Tunataka haki sawa kwa wanyama wote, wakubwa kwa wadogo, wala nyama kwa wala nyasi…”

Simba ambaye alikuwa ndiye mwenyekiti wa mkutano akawajibu: “maneno yenu, enyi Sungura! ni mazuri sana; ila hayana makucha wala meno kama tuliyonayo sisi.”

Hadithi hii inatufundisha nini?
1……………………………………………………………………………………………………………………
2……………………………………………………………………………………………………………………
3……………………………………………………………………………………………………………………
Taja methali, nahau au msemo wa Kiswahili wenye maana inayofanana na maudhui ya hadithi hii;
………………………………………………………………………………………………………………………
………………………………………………………………………………………………………………………
Share:

HADITHI YA SIMBA NA SUNGURA

Simba mwenye njaa, katika pitapita zake za kuwinda, alimkuta Sungura akiwa amelala fofofo. Alishusha pumzi, akatabasamu na kumshukuru sana Mungu kwa ukarimu wake wa kutambua taabiko lake na kumtunuku chakula pasi na haja ya kukitolea jasho.

Taratibu alimsogelea Sungura ili asije akamwamsha, akalala yeye…
Alipoinua miguu yake kutaka kumkamata, mara akatokea Ayala mnono ambaye alipita akikimbia karibu naye, akielekea upande wa kaskazini kwenye uwanda wa nyasi fupi.

 Simba alimwacha Sungura na akakurupuka kumkimbiza yule Ayala.
Vishindo kelele na purukushani za Simba na Ayala vilimgutusha na kumwamsha Sungura ambaye aliamka na kutimua mbio kuelekea upande wa kusini.

Baada ya kumkimbiza Ayala kwa muda mrefu Simba alishindwa na kuamua kurudi ili akamle yule Sungura.
Alipogundua kuwa Sungura naye alikuwa ameamka na kukimbia, Simba alisema kwa kujilaumu, “ama kweli nimepata nilichostahili; kwa kuwa nilikiacha chakula nilichokitia mkononi tayari kwa tamaa ya kutaka kupata zaidi.”

Hadithi hii inatufundisha nini?
1……………………………………………………………………………………………………………………
2……………………………………………………………………………………………………………………
3……………………………………………………………………………………………………………………
Taja methali, nahau au msemo wa Kiswahili wenye maana inayofanana na maudhui ya hadithi hii;
………………………………………………………………………………………………………………………
………………………………………………………………………………………………………………………
Share:

HADITHI YA MTU NA MTI

Mtu mmoja alikwenda kichakani huku akiwa na shoka mikononi kwake, na kuiomba Miti kwa unyenyekevu ili iweze kumpa tawi moja tu dogo ambalo alisema alikuwa na kazi nalo fulani.

Miti ile ilikuwa na tabia njema, ikampa moja ya matawi yake. Kumbe yule mtu alikuwa akihitaji mpini wa shoka lake. Kwa kutumia tawi lile alilopewa akakarabati shoka lake na kisha kuanza kazi ya kuikata Miti ile mmoja baada ya mwingine.

Ndipo Miti ilipon’gamua ilitenda ujinga kwa kiasi gani kutokana na kitendo kile cha kumsaidia adui yao mpini, ambao ulitumika kulitengeneza shoka, ambalo lilitumika kuiangamiza Miti yenyewe.

Hadithi hii inatufundisha nini?
1……………………………………………………………………………………………………………………
2……………………………………………………………………………………………………………………
3……………………………………………………………………………………………………………………
Taja methali, nahau au msemo wa Kiswahili wenye maana inayofanana na maudhui ya hadithi hii;
………………………………………………………………………………………………………………………
………………………………………………………………………………………………………………………
Share:

Live Traffic Feed

Blogroll

BTemplates.com

Inaendeshwa na Blogger.

Jumla ya Mara Iliyotazamwa

Popular Posts

Kumbukumbu la Blogu