Hadithi za kale zenye mafundisho za Esopo zilizoandikwa zaidi ya miaka 3000 iliyopita. Zimetafsiriwa kwa Kiswahili na Issa S. Kanguni, chini ya shirika lisilo la kiserikali la Tanzania Inventors and Techno-Thinkers Consortium (TITC). Tel; +255757242960

Tafuta katika Blogu Hii

Pages

Jumamosi, 31 Mei 2014

KISA CHA NYIGU NA NYOKA

Nyigu alitua kwenye kichwa cha Nyoka na kuanza kumng’ata mfululizo, akimjeruhi vibaya kwa lengo la kutaka kumwua. 
Nyoka, akiwa katika maumivu makali asijue namna ya kujiokoa na adui yake huyo, mara akaona mkokoteni uliojazwa magogo ya miti ukipita. 

Basi kwa makusudi akaamua kwenda njiani na kuweka kichwa chake chini ya gurudumu, akasema, 
“Angalau, mimi na adui yangu tuangamie sote pamoja.”
***

1. Hadithi hii inatufundisha nini?
2. Taja methali au nahau ya kiswahili yenye maana sawa na maudhui ya hadithi hii.
Share:

KISA CHA MITUNGI MIWILI

Mitungi miwili iliachwa kwenye ukingo wa mto, mmoja wa chuma, na mwingine wa udongo. 
Baada ya mvua kubwa kunyesha mbali mto utokako ndipo maji ya mto yalipoongezeka na hatimaye mitungi yote ilisombwa ikaelea kufuata mkondo. 

Basi ule mtungi wa udongo ukawa unafanya jitihada kwelikweli kujiweka mbali na ule wa chuma. Kuona vile, Mtungi wa chuma ukatabasamu na kuuambia ule wa udongo: 
“Usihofu rafiki yangu, mi sikugongi.”


“Sawa, lakini inawezekana nikagusana nawe,” ukasema mtungi wa udongo, “iwapo nitakukaribia; kwani haijalishi wewe ukinigonga, au mimi nikakugonga, nitadhurika tu.”
***
Share:

Ijumaa, 30 Mei 2014

KISA CHA MAADUI WAWILI

Jamaa wawili, ambao walikuwa ni maadui wa kufa na kupona, walijikuta wakisafiri katika merikebu moja. Wakiwa wamepania kukaa mbalimbali kadri iwezekanavyo, mmoja alienda kukaa nyuma kabisa na  mwingine mbele kabisa kwenye ncha ya mwisho ya merikebu. 

Mara kukapiga dhoruba kali na mawimbi yakaanza kukipeleka chombo mrama, na kilipokuwa kwenye hatari ya kuzama, yule jamaa aliyekaa nyuma akamuuliza nahodha ni upande upi wa merikebu ile ungelianza kuzama kabla ya  mwingine. 
Alipomjibu kwamba anaamini ni upande wa mbele utakaozama kwanza, yule jamaa akasema, 
“Kifo hiki hakitokuwa na mateso kwangu, endapo tu nitafanikiwa kumwona yule rafiki yangu pale akitapatapa na kufa kabla yangu.”
***
Share:

KISA CHA PANYA WA MJINI NA PANYA PORI

Panya Pori alimwalika panya wa mjini, ambaye ni rafiki yake kipenzi, amtembelee kwake aje ajionee maisha ya porini. Wakiwa kwenye uwanda wazi wa mashamba, wakila mabaki ya nafaka na mizizi ya miti iliyong’oka, Panya wa Mjini alimwambia rafiki yake, 
 “Huku shamba rafiki yangu unaishi maisha ya wadudu, yaani kama mchwa ama sisimizi, wakati mimi kule nyumbani kwangu ni neema tupu ya vyakula kedekede.  Yaani nimezungukwa na kila aina ya raha na anasa, na iwapo utakubali kufuatana nami nyumbani, kama ninavyoamini utakubali, nawe utapata kufaidi sehemu ya mapochopocho yangu.” 

Kwa maneno yale, Panya Pori akashawishika kiurahisi, na akakubali kuandamana na rafiki yake katika safari ya kurudi mjini. Walipofika, Panya wa Mjini akamtengea rafikiye mlo wa mkate, shayiri, maharagwe, matini yaliyokaushwa, asali, zabibu kavu, na, mwishowe, alimletea kipande kinono cha jibini toka kapuni. Panya Pori, akiwa na furaha isiyo kifani kwa kupata chakula kizuri na kingi kama kile, alishukuru kwa unyenyekevu na kuyalaani maisha yake magumu kule shamba. 

Basi wakiwa ndo wanataka kuanza kula, bwana mmoja akafungua mlango, na wote wawili wakatimka mbio kadri ya uwezo wao na kuingia kwenye kijishimo chembamba kilichowatosha kwa kujibana. Baadaye wakatoka, na kwa mara nyingine kabla hata hawajaanza kula, mtu mwingine akafungua mlango na kuingia kuchukua kitu fulani kabatini, ambapo wale panya wawili, wakiwa na hofu zaidi ya mara ya kwanza, walikimbia na kwenda kujificha tena. 

Mwishowe yule Panya Pori, huku akitweta na akiwa ameshikwa na njaa kwelikweli, akamwambia rafiki yake: 
“Japokuwa umeniandalia mlo maridhawa, sina budi kuondoka na kukuachia uufaidi mwenyewe. Chakula chako kimezungukwa na hatari nyingi mno, siwezi kukifurahia hata kidogo.  Kwangu mimi ni heri maisha ya  kuokoteza nafaka na kuguguna mizizi porini, ambako ninaishi kwa usalama, bila hofu yoyote.”
Akaenda zake.
***
Share:

KISA CHA MBWA WAWILI

Kulitokea bwana mmoja ambaye alifuga mbwa wawili: 
Mbwa mwindaji, ambaye alimfundisha kumsaidia katika kazi zake za uwindaji, na Mbwa mlinzi, aliyemfundisha kulinda nyumba. 

Kila aliporejea nyumbani kutoka mawindoni, alikuwa akimpa yule Mbwa wa nyumbani minofu mikubwa mikubwa ale. Mbwa mwindaji hakupendezwa na jambo lile na alishindwa kuvumilia, alimfuata mwenzie, akamwambia, 

“Ni mateso makubwa kufanya kazi ngumu kama nifanyayo mimi, ilhali wewe, ambaye husaidii lolote katika kuwinda, unajibarizi na kufaidi matunda ya jasho langu.” 

Mbwa wa nyumbani akamjibu, 
“Rafiki yangu, usinilaumu mimi bali umlaumu bwana wetu, ambaye hajanifundisha mimi kufanya kazi bali kuishi kwa kutegemea matunda ya kazi za wengine.”
***
Share:

Alhamisi, 22 Mei 2014

Kisa cha Bwana Mzalendo mwenye Kipawa

Baada ya kufanikiwa kupewa nafasi ya kusikilizwa na mfalme na baraza lake la washauri, Mzalendo mwenye kipaji alitoa karatasi mfukoni mwake, akasema: 
Share:

Jumapili, 18 Mei 2014

KISA CHA TAI, PAKA NA NGURUWE PORI

Kulitokea Tai mmoja ambaye alijenga kiota chake juu ya mti mkubwa; Paka naye, baada ya kuona kuna shimo linalomfaa, alihamia na kuanza kuishi katikati ya shina la mti ule ule; na Nguruwe pia, akiwa na vitoto vyake, akaweka makazi kwenye shimo lililopo wazi chini ya mti ule. 

Basi ikawa Paka, kwa tabia yake mbaya, akaanza kutengeneza hila ili kuvuruga kusanyiko lile la kudra la familia tatu tofauti katika mti mmoja. Ili kutekeleza njama yake, alianza kwa kupanda juu kwenye kiota cha Tai, akamwambia, 
"Ndugu yangu, angamizo linakaribia kushuka juu yako, na mimi pia, kwa bahati mbaya. Jirani yetu Nguruwe-pori, ambaye unamwona kila siku akichimbua chimbua ardhi kwa mdomo wake, anataka kuung'oa mti huu, ili utakapoanguka akamate familia yako na yangu kwa ajili ya chakula kwa watoto wake." 

Baada ya kufanikiwa kumwogofya Tai kiasi kile, Paka alishuka chini kabisa na kwenda kwenye shimo la Nguruwe-pori, akamwambia, "Ndugu yangu, maisha ya watoto wako yapo hatarini; kwani punde tu utakapothubutu kutoka kwenda kutafuta chakula, Tai amejiandaa kushambulia mmoja wa watoto wako, kwa ajili ya chakula cha familia yake." 
Alipofanikiwa kumjaza hofu Nguruwe-pori, Paka akaenda zake kwake na kujifanya kana kwamba naye anajificha kwa woga kwenye shimo lake. Ilipofika nyakati za usiku kila siku alinyata na kutoka kinyemela kwenda kutafuta chakula kwa ajili yake na wanawe, huku akijifanya kuogopa na kuwalinda wanawe mchana kutwa.

Wakati huo, Tai,  akiwa ana hofu kuu dhidi ya Nguruwe-pori, alikaa kwenye kiota chake kutwa kucha, ilhali Nguruwe pori naye, akiwa na hofu kuu dhidi ya Tai, hakuthubutu kutoka kwenye shimo lake. 
Kwa hali hiyo, wote pamoja na familia zao, waliangamia kwa njaa, na kumwacha Paka na wanawe wakijivinjari kwa nafasi.
***
Share:

Live Traffic Feed

Blogroll

BTemplates.com

Inaendeshwa na Blogger.

Jumla ya Mara Iliyotazamwa

Popular Posts

Kumbukumbu la Blogu