Hadithi za kale zenye mafundisho za Esopo zilizoandikwa zaidi ya miaka 3000 iliyopita. Zimetafsiriwa kwa Kiswahili na Issa S. Kanguni, chini ya shirika lisilo la kiserikali la Tanzania Inventors and Techno-Thinkers Consortium (TITC). Tel; +255757242960

Tafuta katika Blogu Hii

Pages

Jumamosi, 17 Mei 2014

KISA CHA MBWA NA MBWA MWITU

Mbwa-mwitu mmoja dhaifu alikuwa akikaribia kufa kwa njaa na mara kwa bahati akakutana na mbwa wa nyumbani ambaye alikuwa akipita. 
"Ah, binamu," alisema mbwa "nilijua tu yatakukuta haya; kwamba maisha yako ya kutangatanga na yasiyo na uhakika ipo siku yatakuangamiza. Kwanini usifanye kazi maalum na ya uhakika kama nifanyavyo mimi, ili upate chakula kila mara kama nipatavyo  mimi?" 
"Nakubaliana na wewe kabisa ndugu yangu," alijibu Mbwa-mwitu, "endapo tu nikipata nafasi." 
"Nafasi sio tatizo, mi ntakufanyia mpango," alisema Mbwa; "twende nami nyumbani kwa bwana wangu na nitamwomba akuajiri tufanye kazi pamoja nami." 

Basi Mbwa-mwitu na Mbwa wakaongozana kuelekea mjini. Wakiwa bado njiani, wanakaribia kufika Mbwa-mwitu akagundua kwamba nywele kwenye sehemu fulani ya shingoni ya Mbwa zimenyonyoka na kubaki chache, hivyo akamuuliza Mbwa kulikoni. 
"Oh, wala si kitu," Mbwa alijibu. "Hii ni sehemu ambayo mkanda wa nyororo hufungwa nyakati za usiku ili kunifanya nibaki sehemu moja; unauma na kukera kidogo, ila baada ya muda unazoea." 

"Ha ndiyo hivyo?" alisema mbwa mwitu. "Basi kwaheri ndugu yangu, Bwana Mbwa."
***
Share:

KISA CHA MBWA NA SUNGURA

Mbwa mwindaji alimvumbua Sungura kwenye mafukutu juu ya kilima na kuanza kumkimbiza kwa kitambo, wakati fulani alimkaribia na kung'ata kwa nguvu kwa meno yake makali kana kwamba ataka kumuua, na mara nyingine alimkumbatia kana kwamba anacheza na mbwa mwenzake.

 Yule Sungura akamwambia, "natamani ungekuwa mkweli kwangu, na kuonyesha dhamira yako halisi. Kama we ni rafiki, kwa nini umening'ata kiasi hiki? na kama we ni adui, kwa nini basi unacheza nami?"
***
Share:

KISA CHA MZEE KIPARA NA MBUNG'O

Mbung'o alitua kichwani kwa Mzee mmoja na kumng'ata kwenye sehemu yenye kipara, ambapo yule Mzee kwa kutaka kumwangamiza Mbung'o alijipiga kofi pwaaa! 

Yule mbung'o alifanikiwa kukwepa na aliondoka akisema kwa dhihaka, 
"Ulipanga kulipiza kisasa, hata kwa kuua, maumivu madogo tu ya kung'atwa na mdudu kama mimi, ona sasa ulivyojitenda na kujiongezea maumivu juu ya maumivu?"

 Mzee kipara akamjibu, 
"Ni rahisi kwangu kujisamehe maumivu ninayojipa mwenyewe, kwani najua hakukuwa na nia ya kujiumiza. Lakini wewe, mdudu baradhuli mwenye tabia ya kunyonya damu za watu, natamani ningelifanikiwa kukuua hata kama ningalipata maumivu makubwa zaidi ya haya niliyopata sasa."
***

Share:

KISA CHA MAMA NA MTETEA

Hapo zamani za kale kulikuwako mama mmoja ambaye alikuwa na kuku wake mtetea aliyetaga yai moja kila siku.

 Kila wakati yule mama alifikiri na kujiuliza atawezaje kupata mayai mawili kwa siku badala ya moja, na mwishowe, ili kutimiza azma yake, akaamua kuanza kumlisha yule kuku mara mbili ya shayiri za chakula alichokuwa akimpa kwa siku.

Basi kuanzia siku hiyo yule kuku alinenepa
sana na kuwa mtepetevu, na hakutaga tena.
***

Share:

KISA CHA MBWEHA ALIYEKATWA MKIA

Hapo zamaini za kale, kulitokea Mbweha mmoja mjanja. Siku moja kwenye pitapita zake kwa bahati mbaya alinaswa mtegoni, na katika kuhangaika alifanikiwa kujinasua, ila alikatika mkia ukabakia kipisi kifupi tu.

Siku za mwanzo mwanzo aliona aibu kujionyesha ulemavu wake wa kutokuwa na mkia kwa mbweha wenzake. Baadaye akaamua kujibaraguza na kufanya kana kwamba kukosa mkia si kitu, akawaalika Mbweha wote kwenye mkutano mkuu, ili wajadili pendekezo alilo nalo moyoni.

Walipokusanyika, Mbweha alitangaza pendekezo lake, kwamba eti mbweha wote ni vyema wakakata mikia yao na kubaki na vipisi kama yeye.  Akasema kwamba mkia ni mzigo wanapokuwa wanafukuzwa na maadui zao, mbwa; na pia unasumbua wanapohitaji kuketi kitako wazungumze mambo kirafiki na wenzi wao. Akapaza sauti na kudai kuwa haoni faida yoyote ya wao kuendelea kubeba zigo la mkia usio na tija yoyote.

“Hiyo ni sawa kabisa,” akajibu mbweha mmoja mzee; “ila sidhani kama ungelitoa pendekezo la kukata mikia ambayo ni kifaa chetu muhimu, laiti kama wewe mwenyewe usingalipatwa janga la kupoteza mkia wako.”
***
Share:

Jumatano, 7 Mei 2014

KISA CHA MBWEHA, MBWA MWITU NA NYANI

Mbwa mwitu alimshutumu  vikali Mbweha kwa kumwibia, ila Mbweha alikana katukatu kwamba hakutenda kosa hilo. Baada ya kuzozana kwa muda, wakampelekea Nyani shauri hilo ili atoe hukumu na kumaliza mgogoro baina yao. 

Basi baada ya kila mmoja wao kupewa nafasi ya kujieleza kwa kina, Nyani akatangaza hukumu ifuatayo: 
"Siamini katu kwamba wewe, Mbwa mwitu, umepotelewa na hicho unachodai kuibiwa; na ninaamini kabisa kwamba wewe, Mbweha, umeiba hicho unachokataa katakata kuwa hujaiba."
***

Hadithi hii inatufundisha nini? Jibu ujishindie.
Share:

KISA CHA WASAFIRI WAWILI NA SHOKA

Jamaa wawili walikuwa wakisafiri pamoja. Wakiwa njiani mmoja wao aliokota shoka zuri lililokuwa limelazwa kando ya njia, akalichukua na kusema, 

"Nimeokota shoka." 
"Hapana rafiki yangu," mwenzake alimjibu, "usiseme 'Nimeokota' bali 'Tumeokota' shoka." 

Basi kabla hata hawajafika mbali wakamwona mwenye shoka lake akiwafuata kwa hasira, ndipo yule aliyeliokota shoka akasema, "Duh! tumekwisha." 

"La hasha," alijibu yule mwenzake, "endelea na ile kauli yako ya awali, rafiki yangu; kile ulichoona sahihi wakati ule, kione kuwa sahihi hata sasa. Sema 'Nimekwisha', sio 'Tumekwisha'."
***
Share:

Live Traffic Feed

Blogroll

BTemplates.com

Inaendeshwa na Blogger.

Jumla ya Mara Iliyotazamwa

Popular Posts

Kumbukumbu la Blogu