Onyo; Hadithi hii ni ya kubuni (fiction) na haina uhusiano na tukio lolote lililowahi kutokea. Majina ya wahusika na tabia zao hazina uhusiano na mtu yeyote halisi hivyo ikitokea aina yoyote ya kufanana ni bahati mbaya tu.
Mtunzi; Issa S. Kanguni
0757242960 / 0655242960
ibot.isk@gmail.com
Haki zote zimehifadhiwa.
Chapter One
Sauti
na kikiri kakara toka chumba cha pili zilimshtua kutoka usingizini. Alitupa
shuka kando, akajiviringisha upande na kujiinua kiwiliwili. Akafikicha macho
kwa mkono wa kushoto na kushusha miguu chini kabla ya kunyanyuka na kusimama wima huku vifundo vya miguu vikaalika na mapaja yake laini kusisimka. Alipapasa kiberiti
awashe kibatari akasita. Akiwa mtupu vilevile bila kujisitiri alitembea kwa kunyata
hadi mlangoni kuhakiki kama kweli jana kabla ya kulala aliufunga kwa komeo. Aliporidhika akatembea
tena kwa kunyata hadi kwenye kidirisha kidogo upande wa pili wa chumba chake.
Akachungulia nje. Bado giza... hakujapambazuka. Nyimbo hafifu za ndege zilizosikika
toka mabondeni mbali zilimpa hakika kwamba pambazuko lilikuwa limekaribia. Kiupepo
cha ubaridi kilipuliza kuashiria mwanzo wa msimu wa kipupwe.
Nia yake ilikuwa ni kuondoka kukiwa bado giza
na alijua ana dakika chache tu zakujiandaa na kutoka, vinginevyo mpango mzima ungelivurugika.
Maandalizi
ya kila kitu alishayafanya tangu usiku kabla ya kulala. Giza lilijaribu kumzuia
asione, halikufanikiwa.
Alisogea kitandani akafunua godoro
mchagoni na kulishikilia kwa mkono wa kushoto huku mkono wa kuume ukipapasa
papasa na hatimaye kutoa kitita cha nguo zilizokunjwa vizuri. Harakaharaka
akashusha godoro na kuanza kuvaa. Alianza boxer mpya nyeupe yenye urembo wa
kung’aa ng’aa na picha ya mkuki moyoni, halafu suruali ya jinsi nyeusi ya kubana,
akafunga mkanda. Kisha akavaa sidiria tatu, ya kwanza nzito nyeupe, ya pili
nyeupe tena na ya tatu nyeusi. Zilimkaa vyema. Halafu akaikunjua na kuivaa blauzi ya rangi ya
kijivu yenye madoadoa ya pinki na mikunjo shingoni, na baada ya hapo akavaa
wigi lenye nywele ndefu kichwani. Alipomaliza, alikuwa na mwonekano wa msichana wa miaka mitana zaidi ya umri wake. Just how she wanted!
“Leo ndio leo…” alijisemea
kimyakimya “ama zao ama zangu. Kama wanajifanya wao ndo wanajua mapenzi sasa
leo ndo mwisho wao.”
Aliinama akafungua kishubaka cha
kitanda na kutoa vifaa vyake vya kazi, kibunda cha pilipili ya unga, nyembe
tatu mpya, na kifaa maalum alichokibuni na kukiunda mwenyewe na kukiita kwa
kifupi FZ (anatamka efzii), akaviweka kwenye mkoba mweusi pamoja na miwani ya
giza, mtandio na kamba ya nailon.
Alivaa
raba, akafunga gidamu. Alisimama akajinyoosha na kujiweka sawa. Aliuweka mkoba
begani na kutembea kwa uangalifu hadi mlangoni, akanyoosha mkono ili afungue,
mara akasikia mlango wa chumba cha pili unafunguliwa. Akasubiri.
“Hapa leo huendi… kama hutaki twende
wote huendi…” sauti ya mwanamke ilisikika ikisema kwa kulalamika.
“Haya… mdomo si mali yako. Lalama
weeee, mwisho wa siku mi siwezi kukatisha safari yangu.” Mwanaume alijibu
taratibu kwa dharau.
“Twende sote… kwani kuna tatizo gani
tukienda sote?” alihoji mwanamke.
“Kwani n’kienda peke yangu kuna
tatizo gani?”
“Kuna tatizo gani!... yaani unauliza
kuna tatizo gani? Kwani we hujui? …huendi. La kama uk’enda peke yako basi
usichukue pesa zote, chukua nusu.”
“Ili?”
“Ukienda na pesa zote ndo haurudi
tena wewe… hadi ziishe..”
“Unaota wewe…” akamsonya “…
unajifanya unataka kunilinda mimi utaweza wapi… nipishe huko. Unasahau ni nani
kamwoa mwenzie humu ee… sasa kwa taarifa yako… ipo’ivi… kadri unavyozidi
kujifanya unanipangia masharti ndo kwanza unazidi kunichefua. Kwa mfano,
nilipanga kuacha kiasi cha pesa sasa…” ilisikika sauti ya zipu ikifunguliwa kwa
nguvu “…nachukua zote. Funga domo lako. Na umesema sitorudi hadi ziishe… well…
omba mungu…”
“Lakini kwa nini mume wangu
unanifanyia hivi!... mbona unapokuwa huna pesa tunakaa vizuri… sasa…”
“Aaagh… haukomi tu na mahubiri yako we
mwanamke… sasa leo n’takuonyesha… na tena ndo kwanza unasababisha n’ondoke
kabla ya mawio. N’mekuchoka… mwanamke gani wewe… sura mbaya na gubu haviendi…
afu tena unasahau sheria inaniruhusu kuwa na wangapi.”
“Lakini kumbuka tulikotoka mume
wangu.”
“Tulikotoka?... ipo’ivi… sahau
tulikotoka. Ndo’ubovu wa uchumba wa kushinikizwa na wazazi… we kwa akili yako
unadhani kosa kushinikizwa ni n’ngekuoa wewe na matege kama hayo!? No. na hata
kama n’ngekuoa ingelikuwa ni kwa maamuzi yangu mwenyewe si kwa shuruti ya
wazazi kisa etu una tabia njema… haya sasa tabia njema i wapi leo...”
Mwanamke alijaribu kusema jambo
akashindwa. Akaanza kulia kwa uchungu. Ni dhahiri haikuwa mara yake ya kwanza
kusemwa na kutendwa vibaya katika ndoa yake, ila kudharauliwa kulimuuma sana. Na
mume wake hakuwa mwepesi wa kuinua mkono kupiga, bali ulimi. Mara zote alilenga
kujeruhi moyo, si mwili. Alisikika akijitupa chini na kuanza kulia… kilio cha
yaliyopita, yaliyopo, na yajayo.
Mlango ukabamizwa, sauti ikakoma. Nyayo
zilisikika zikipita kwenye ususu kwa haraka kisha mlango wa kutokea nje
ukafunguliwa, halafu baadaye ule wa maliwatoni.
Alijua kinachoendelea nje. Alijua
anachopaswa kufanya.
Bila
kupoteza muda, hasira zake zikiwa zimeongezeka maradufu, alifungua mlango
akatoka na kuufunga nyuma yake. Alipiga hatua ndefu ndefu na kufika kwenye mlango
wa nje ambao uliachwa wazi akachungulia nje kwa tahadhari kisha akainama na
kutoka taratibu. Sekunde chache baadaye alijikuta uchochoroni nje ya nyumba
kukiwa bado na giza. Hasira na chuki dhidi ya baba yake, na huruma na upendo
kwa mama yake vilisaidia kumwondoa woga ingawa ilikuwa ndo mara yake ya kwanza
kutoka nyumbani kwao katika muda na staili kama ile. Mawingu yalianza kujongea
kugubika anga na kufanya giza liwe totoro. Akatafuta sehemu nzuri ya kujibanza
kando ya barabara chini ya mti. Sauti kali ya bundi ilisikika ikitokea kwenye
moja kati ya miti mitatu mikubwa jirani na pale alipojificha. Hakujali.
“Leo
ndo leo… ama zao ama zangu.” Alijisemea tena kwa sauti yenye hisia kali ya
kisasi na kupania. Alifungua pochi kutoa mtandio huku akiangaza kila upande,
akajitanda na kuketi kwenye kigingi. Akasubiri…
Itaendelea....
0 maoni:
Chapisha Maoni