Hapo zamani za kale kulikuwepo mvulana
mmoja aliyeishi na mama yake. Siku moja, akiwa shuleni kijana
aliiba kitabu cha mwanafunzi mwenzake na kurudi nacho nyumbani
akamwonyesha mama yake. Yule mama, sio tu hakumchapa wala kumgombeza,
bali alimpongeza.
Kijana akakua kuelekea utu uzima, huku akiendelea
na tabia yake ya wizi wa vitu vikubwa zaidi.
Wanasema za mwizi arobaini. Mwishowe ilitokea siku akakamatwa akijaribu kutaka kuiba, na akiwa amefungwa mikono yake
kwa nyuma na wananchi wenye hasira, akapelekwa kwenye uwanja maalum ambapo wahalifu hupewa
adhabu ya kunyongwa hadharani.
Mama yake naye akafuata msafara akilia na kujipigapiga kwa huzuni na uchungu wa
mwanaye, ambapo yule kijana kuona vile akasema, “Naomba kuongea na mama yangu
nimnong'oneze jambo tafadhali.” Mama yake akamsogelea kumsikiliza.
Basi yule kijana alimng'ata sikio kwa nguvu nusura anyofoe kipande.
Mama yake akamfokea na kumtolea maneno
ya kumlaani kwamba ni mtoto mbaya, naye akajibu “Ah! Laiti
ungalinichapa na kunikemea siku ya kwanza nilipoiba na kukuletea kile
kitabu, yasingenifika haya, na wala nisingalikufa kifo cha aibu kama
hiki.”
***
0 maoni:
Chapisha Maoni