Siku moja Mbweha alitumbukia kisimani kwa bahati mbaya, na
ingawa kisima chenyewe hakikuwa na kina kirefu sana, alijikuta akishindwa kutoka nje tena.
Baada ya kuhangaika kwa muda mrefu bila mafanikio, hatimaye akatokea Beberu
mwenye kiu kali. Beberu alidhani kuwa Mbweha ametumbukia kwenda kunywa maji
kukidhi kiu yake, na hivyo akauliza kama maji yalikuwa safi au la.
“Ni safi na matamu kupita maji yote kwenye
nchi hii,” alijibu Mbweha yule mjanja, “jirushe utumbukie ujionee mwenyewe. Maji
ni mengi yanatutosha sote na tutasaza.”
Beberu mwenye kiu mara moja alijitosa
kisimani na kuanza kuyafakami maji. Mbweha naye kwa haraka sana alimdandia Beberu
mgongoni akachupa kwenye ncha za pembe za Beberu na kutoka zake nje ya kisima.
Yule Beberu mpumbavu akang’amua kuwa
amejiingiza matatizoni, akaanza kumbembeleza Mbweha amsaidie kumtoa kisimani.
Lakini Mbweha tayari alikwishaanza kutokomea zake mitini.
“Laiti ungalikuwa na akili kama
ulivyo na ndevu, rafiki,” alimwambia huku akikimbia zake, “ungalikuwa makini na
kujaribu kung’amua kwanza njia utakayoitumia kutokea kisimani kabla
hujatumbukia.”
Mwisho.